Mahakama ya Juu Yamulikwa Na Viongozi Wa Kenya Kwanza
Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula, amekuwa kiongozi wa hivi punde zaidi wa ngazi ya juu wa serikali kukosoa Mahakama ya Juu kuhusu uamuzi wake wa kusajili mashoga na wasagaji almaarufu LGBTQ.
Mahakama ya Juu mnamo Februari 24, iliamua kwamba mamlaka ya Kenya ilikosea kupiga marufuku jumuiya ya mashoga kusajili shirika la haki.
Wetangula katika taarifa yake, ameikashifu Idara ya Mahakama akibainisha kuwa ilikuwa na wajibu wa kudumisha maadili ya nchi.
Kauli ya Wetangula inajiri siku moja baada ya Mwanasheria Mkuu Justin Muturi kutangaza kwamba atapinga uamuzi wa Mahakama ya Juu kuruhusu usajili wa LGBTQ kama Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs).
Huku akitofautiana na uamuzi huo, Muturi amesema kuwa Wakenya wanapaswa kuruhusiwa kutoa maoni yao kuhusu suala la LGBTQ kwa vile lina uzito wa maisha.
Aidha, amesema mjadala wa usajili wa vikundi vya LGBTQ unapaswa kuletwa kanisani kwa mjadala.
Kanisa kwa upande wake limetofautiana vikali na uamuzi huo likisema kuwa unamomonyoa maadili ya nchi.
Askofu Mkuu Arthur Kitonga wa Redeemed Gospel Churches of Kenya aliteta kuwa nchi ingelaaniwa ikiwa mchakato wa usajili wa vikundi vya LGBTQ ungefuatwa.
Maoni yake yaliungwa mkono na askofu msimamizi wa CITAM Calisto Odede, ambaye alitoa maoni kuwa tuko katika hatari ya kuruhusu sheria zingine zisizo za kimaadili nchini.
Mbunge wa Homa Bay Town George Kaluma alisema kuwa atawasilisha mswada bungeni unaoharamisha mapenzi ya jinsia moja.