Mahakama itaanzisha mahakama mpya huko Yala, Kaunti ya Siaya
Mahakama ya juu itaanzisha mahakama mpya katika eneo ya Yala, Kaunti ya Siaya kama sehemu ya juhudi zake za kuhakikisha mabadiliko ya kijamii kupitia upatikanaji wa haki, Msajili Mkuu wa Idara ya Mahakama Anne Amadi amesema.
Amadi, ambaye alikagua jengo lililotolewa na serikali ya Kaunti ya Siaya huko Yala pamoja na Gavana James Orengo alisema sheria inaitaka mahakama kuwa na mahakama katika kila kaunti ndogo hivyo basi msaada kutoka kwa serikali ya kaunti hiyo utasaidia kutimiza lengo lake.
Msajili mkuu alisema kuwa wataanzisha mahakama ndogo ya madai ya hadi Ksh 1 milioni akiongeza kuwa mahakama hiyo itawaokoa wakazi wa Gem muda na pesa ambazo wamekuwa wakitumia kusafiri hadi Siaya au Mahakama ya Sheria ya Maseno kutafuta haki.
Aidha Aliipongeza Serikali ya Kaunti ya Siaya kwa kuunga mkono kuanzishwa kwa mahakama hiyo, na kuongeza kuwa mahakama itarekebisha jengo hilo ili kuendana na mahitaji yake kabla ya kutuma wafanyikazi.
Gavana wa Siaya, James Orengo alisema kitengo cha ugatuzi kitashirikiana na mahakama ili kuhakikisha kuwa wakazi wa eneo hilo wanapata huduma za mahakama.
Alisema kuwa ni kwa nia ya kutilia mkazo kanuni hiyo ambapo serikali ya kaunti ilifikia hitimisho la kuanzisha mahakama huko Yala.