Home » Kwa Nini Aliyekuwa Waziri Matiang’i Alishindwa Kuheshimu Wito Wa DCI…?

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Dkt. Fred Matiang’i ameshindwa kufuata wito uliotolewa na Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kumtaka ajitokeze kuhojiwa kuhusu madai ya kuvamiwa na polisi nyumbani kwake wiki mbili zilizopita.

 

Hii ni baada ya afisa mkuu wa Polisi Michael Sang Alhamisi kutoa agizo la kumshinikiza Matiang’i kufika katika makao makuu ya DCI leo Ijumaa asubuhi, bila kukosa, kwa msingi kwamba alichapisha habari za uwongo kuhusiana na madai ya uvamizi wa polisi wiki mbili zilizopita.

 

Akizungumza nje ya Mahakama ya Milimani leo Ijumaa, wakili wa Matiangi Danstan Omari, ametupilia mbali madai hayo akibainisha kuwa si waziri huyo wa zamani na wawakilishi wake wa kisheria waliopokea maagizo kama hayo.

 

Kulingana na wakili huyo mwenye uzoefu, sheria inashurutisha mashirika ya uchunguzi kuwasilisha wito ana kwa ana kwa watu ambao inawalenga kuhojiwa lakini haikuwa hivyo Sang alipotoa maagizo yake.

 

Omari ameongeza, pia kuwa sheria inasema kwamba hati za wito zinapaswa kusainiwa na kushuhudiwa na angalau maafisa watatu waandamizi wa polisi na kwamba timu ya kisheria ya walengwa wa wito huo inapaswa kuthibitisha kupokea maagizo kwa maandishi.

 

Huku akibainisha kuwa amri ya Mahakama Kuu ya kumzuia DCI kumkamata Matiang’i haimzuii kuchunguzwa na shirika hilo, Omari alikashifu DCI kwa kutofuata taratibu za jinsi wito unavyofaa kutolewa.
Ameongeza kuwa iwapo DCI itafuata mwongozo uliowekwa kuhusu wito, Matiang’i atajitokeza kwa hiari kuhojiwa.

 

Omari hakufichua aliko Matiang’i ambaye hajaonekana hadharani kufuatia madai ya uvamizi huo, lakini alifichua kuwa amekuwa akiwasiliana mara kwa mara na waziri huyo wa zamani ambaye anasema bado yuko salama kwa sasa.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!