MCK Yapinga Mashambulizi Ya Serikali Dhidi Ya Vyombo Vya Habari Baada Ya Matamshi Ya DP Gachagua
Baraza la Vyombo vya Habari nchini (MCK) limeibua wasiwasi kuhusu kuendelea kushambuliwa kwa vyombo vya habari na maafisa wa serikali likisema linahujumu jukumu lake kwa umma.
Katika taarifa leo Ijumaa, Mkurugenzi Mtendaji wa MCK David Omwoyo amewaonya viongozi wa kisiasa dhidi ya kukosoa vyombo vya habari katika mikutano ya hadhara akisema vinawaweka wanachama wake katika hatari ya kushambuliwa kimwili na kuondoa imani katika jukumu lake kama mlinzi wa jamii.
Ameongeza kwamba “Viongozi wanapowashambulia waandishi wa habari, inaweza kuondoa imani ya umma kwa vyombo vya habari kwa kujenga hali ya kutoaminiana na kuwashuku waandishi wa habari.
Hili linaweza kusababisha maswali kuhusu usahihi na usawaziko wa kuripoti habari, jambo ambalo ni muhimu ili kudumisha uraia wenye ujuzi.”
Huku akiitaja hatua hiyo kuwa ”ya kutisha kwa wanahabari”, Omwoyo amesema kuwa baadhi ya hisia dhidi ya vyombo vya habari na maafisa wa Serikali ni njama ya kuvuruga umma kutokana na masuala muhimu yanayowahusu.
Ameonya viongozi wa serikali kujiepusha na vitisho akisisitiza kuwa ni sawa na kujaribu kunyamazisha vyombo vya habari.
“Baraza linawataka viongozi kuacha kuwatisha waandishi wa habari na kuwakatisha tamaa kuripoti habari muhimu jambo ambalo linadhoofisha uwezo wa vyombo vya habari kutimiza wajibu wake katika jamii, tunaamini kuwahujumu wanahabari ni kuwakatisha tamaa na kuacha mambo muhimu yanayohitaji umakini na kuchukuliwa hatua. ,” maneno ya Omwoyo.
Kutokana na hali hiyo, baraza hilo limewataka viongozi wa kisiasa kushughulikia rasmi kutoelewana na vyombo vya habari badala ya kutoa picha mbaya ya wanahabari mbele ya umma.
Matamshi ya MCK yanakuja mwanzoni mwa maoni ya Naibu Rais Rigathi Gachagua mnamo Alhamisi, ambapo alishutumu baadhi ya vyombo vya habari kwa kufadhiliwa na wale aliowataja kuwa ‘makundi ya maziwa’ ili kumkemea.
“Kama hatukuogopa Uhuru na system na deep State, watu wa magazeti tutaogopa nyinyi? Mwache hiyo maneno mko nayo. Mnakuja hapa Murang’a mkutano mzuri mnakoroga mnaweka uwongo, mpaka huyu [Murang’a Senator Joe] Nyutu sasa anatoa jasho eti hakusema. Usijisumbue kuhusu watu hawa Nyutu, sahau kuhusu wahusika hawa,” alisema.