Boni Khalwale: Nafahamu Viongozi Wa ODM Waliosusia kwenda mkutano Wa Raila Jevanjee

Seneta wa Kakamega Boni Khalwale ameibua hisia mseto kuhusiana na mkutano wa Azimio la Umoja one-kenya uliofanyika jana Jumatano, akisema uliporomoka vibaya.
Huku akidai kuwa anafahamu baadhi ya viongozi wanaoegemea upande wa (ODM) ambao walisusia mkutano huo, Seneta Khalwale amesema sasa ni dhahiri kwamba muungano huo “utasambaratika” hivi karibuni.
Aidha amedai kuwa mtindo wa Raila wa kufanya siasa umekuwa wa uzee na “umekaribisha kanuni ya uchovu wa siasa”.
Akifichua majina ya watu “waliosusia” kuhudhuria mkutano huo, Khalwale amesema kuwa ODM inazidi kuwa kifaa butu siku moja baada ya nyingine huku wanachama wengi wakionekana kusitisha uhusiano wao na chama hicho.
Wanachama aliowataja ni pamoja na Mbunge wa Homa Bay George Kaluma, mwenyekiti wa ODM John Mbadi, aliyekuwa mbunge wa Kibra Imran Okoth na mbunge wa Budalangi Raphael Wanjala.
Wengine wandani wa Raila waliosusia ni pamoja na Gideon Ochanda wa (Bondo), Elisha Odhiambo wa (Gem), Mark Nyamita wa (Uriri), Caroli Omondi wa (Suba Kusini), Shakeel Shabir wa (Kisumu Mashariki, ) Felix Odiwuor almaarufu Jalang’o wa (Lang’ata), Paul Abuor wa (Rongo), John Owino wa (Awendo) na Seneta wa Kisumu Tom Ojienda.