DPP Apewa Siku 15 Kuwasilisha Ripoti Kuhusu Kesi Ya Dereva Ra Rally Maxine Wahome
Mkurugenzi wa mashtaka ya umma ODPP na afisa wa uchunguzi wamepewa siku 15 kuandikisha ripoti kuhusu jinsi kesi dhidi ya dereva wa masafa marefu Maxine Wahome inapaswa kuendelea.
Hii ni baada ya hakimu Bernard Ochoi kuamua kwamba maombi mseto ambayo yaliwasilishwa kortini mwaka jana hayawezi kufungwa bila kuwasilisha matokeo mbele ya mahakama.
Ochoi alisema kuwa itakuwa dhuluma kwa mahakama ikiwa ombi hilo mseto lingefungwa bila matokeo hayo.
Vile vile, mahakama iliagiza kwamba mali aliyokuwa akiishi Maxine na mpenzi wake marehemu Asad Khan, ambayo ilikuwa imetiwa alama kuwa eneo la uhalifu itolewe kwa mwenye nyumba katika muda wa siku tano zijazo.
Maxine alifikishwa kortini kwa mara ya kwanza mnamo Desemba 2022, baada ya madai ya ugomvi kati yake na Khan, ambapo baadaye alijeruhiwa vibaya na baadaye kufa.