Home » “Ni Aibu Kuona Magavana Wa Zamani Wakigombea Nyadhifa Za CAS,” Wabunge Wasema.

“Ni Aibu Kuona Magavana Wa Zamani Wakigombea Nyadhifa Za CAS,” Wabunge Wasema.

Wabunge Robert Mbui wa (Kathiani) na Sylvanus Osoro wa ( Mugirango Kusini) wameibua wasiwasi kuhusu wagombeaji 224 walioteuliwa kuwa Katibu Mkuu Tawala (CAS).

 

Akiongea kwenye kipindi cha runinga moja humu nchini leo hii asubuhi, Mbunge Mbui amesema kuwa inashangaza kuona viongozi na wanachama wa zamani walioshindwa katika uchaguzi wa Agosti 2022 wakiwania nyadhifa hizo na tayari wamefurahia marupurupu ya uongozi.

 

Kulingana na mbunge Mbui, nyadhifa hizo zinafaa kupewa vijana ambao hawajahudumu katika utumishi wa umma kwa ajili ya vizazi vya maendeleo ya taifa.

 

Mbunge Mbui ameendelea kutoa maoni kuwa viongozi wa Kenya ambao wameondoka madarakani wanapaswa kuwa tayari kujitosa katika taaluma nyingine mbali na siasa na kuongeza kuwa nyadhifa za uwaziri zinafaa kutolewa kwa watu wengine, ikiwezekana vijana wa Kenya, ili kuhimiza ukuaji.

 

Kwa upande wake, Mbunge Osoro ametoa maoni kwamba waliokuwa magavana hawapaswi kuangalia nyadhifa za CAS, akidai kuwa tayari wametumia fursa zote za kuwatumikia wananchi na hawatakuwa na thamani yoyote katika nyadhifa za uwaziri.

 

Aidha amekariri maoni ya Mbunge Mbui kuwa nyadhifa hizo badala yake zipewe vijana.

 

Wagombea 224 wameorodheshwa na Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) Jumatatu jioni na watatarajiwa kufika kwa usaili kuanzia Machi 1, 2023.

 

Baadhi ya majina mashuhuri yaliyowasilishwa kwa nafasi hizo ni pamoja na:

 

Kasisi wa jiji na aliyekuwa mgombea wa ugavana Nairobi Margaret Wanjiru, Aliyekuwa Mbunge wa Soy Caleb Kositany, Aliyekuwa Mbunge wa Jubilee Gideon Keter na Aliyekuwa Mtaalamu wa Mikakati wa Kidijitali katika afisi ya Naibu Rais wa wakati huo William Ruto, Dennis Itumbi.

 

Watu wengine ni pamoja na Aliyekuwa Seneta Mteule Isaac Mwaura, Aliyekuwa Seneta Mteule Millicent Omanga, Aliyekuwa mwanahabari Mwanaisha Chidzuga, Aliyekuwa Katibu Mkuu wa KNUT Wilson Sossion, Aliyekuwa Mwakilishi wa Wanawake wa Kirinyaga Wangui Ngirici na Aliyekuwa Gavana wa Samburu Moses Lenolkulal.

 

Mwanahabari wa zamani Bonnie Musambi pia alikuwa miongoni mwa walioteuliwa pamoja na Mwanasoka McDonald Mariga Wanyama, Aliyekuwa Seneta Mteule Mary Yiane, Aliyekuwa Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri, Aliyekuwa Seneta wa Lamu Anuar Loitiptip, Aliyekuwa Mbunge wa Starehe Charles Njagua, almaarufu Jaguar miongoni mwa wengine.

 

Wananchi pia wamealikwa kuwasilisha taarifa zozote za kuaminika kuhusu wagombea walioteuliwa.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!