Winnie Odinga Aunga Mkono Uamuzi wa Ruto Kubadilisha Maagizo ya Uhuru

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Winnie Odinga ameunga mkono uamuzi wa Rais William Ruto wa kuondoa marufuku ya awali iliyowekwa kwa bidhaa za maziwa ya Uganda na mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta.
Katika Mahojiano na Televisheni moja nchini Uganda, Winnie ameonyesha kwamba kwa vile Kenya na Uganda ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kulikuwa na haja ya kuongezeka kwa ushirikiano.
Kulingana na Mbunge wa EALA, kuinua viwango kunahitaji mbinu shirikishi, na kuondoa marufuku hayo ilikuwa hatua muhimu ya kufikia ushirikiano huo.
Aidha amedokeza kuwa uamuzi wa Uhuru mnamo 2021, ulizua mtafaruku kati ya Kenya na Uganda.
Mbunge huyo ameteta kuwa kwa mtazamo wa wakulima wa Kenya, gharama ya uzalishaji ni ya juu kiasi, na bidhaa zilizomalizika haziwezi kushindana na bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.
Winnie ameonyesha kuwa mazungumzo hayo yanapaswa kuzingatia uchumi wa kiwango badala ya marufuku na vizuizi.
Ikumbukwe kwamba Babake Winnie, aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, aliapa kutoitambua serikali ya Rais William Ruto.
Raila alishikilia kuwa Ruto yuko afisini kinyume cha sheria na amefanya mikutano kadhaa dhidi ya serikali.
Aliyekuwa rais Uhuru Kenyatta alisisitiza zaidi kumuunga mkono Raila, licha ya kushinikizwa kutambua utawala uliopo.
Wakati uo huo, Waziri wa Biashara, Moses Kuria, alikuwa amedokeza kuhakiki uagizaji wa mayai ya Uganda.
Kuria aligusia masuala hayo alipokuwa akipimwa kwa wadhifa huo Oktoba 2022.