Home » Kisumu: Chifu Ahamasisha Zaidi Ya Familia 150 Za Mitaani Kupata Vitambulisho

Kisumu: Chifu Ahamasisha Zaidi Ya Familia 150 Za Mitaani Kupata Vitambulisho

Zaidi ya watoto 150 wa mitaani mjini Kisumu wanatazamiwa kupokea vitambulisho vya kitaifa kufuatia kampeni yenye mafanikio ya Chifu Msaidizi wa Eneo la Kaskazini John Migun.

 

Maarufu kama chifu wa densi baada ya video zake kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, Migun ametumia umaarufu huo kuwafikia watoto wa mitaani wenye umri wa miaka 18 na zaidi ili kupata hati hiyo muhimu.

 

Kuhusu Vijana wa mitaani, amesema, watachunguzwa ili kuhakikisha kuwa kweli wana sifa za kupewa vitambulisho kama inavyotakiwa kisheria.

 

Migun amesema kuwa zoezi hilo linalotekelezwa kwa ushirikiano na mashirika ya Homeless of Kisumu linalenga kuwaondoa watoto hao mitaani na kuwasaidia kupata ajira ya maana.

 

Kadi hizo amesema zitawawezesha watoto hao wa mitaani kupata huduma mbalimbali za serikali ikiwamo huduma bora za afya na elimu.

 

Aidha ameongezea kuwa jambo hilo, litasaidia kukabiliana na ongezeko la visa vya ukosefu wa usalama katika eneo hilo ambapo magenge ya wanaotumia panga yameacha hali ya hofu miongoni mwa wakazi.

 

Kwa kuungwa mkono na serikali ya kaunti, vijana hao wa mitaani, amesema, watapewa barua za mapendekezo ili kuwawezesha kupata kazi za kusafisha na kupakia na wakati huo huo kufanya kazi katika maduka makubwa na viwanda katika eneo hilo.

 

Victor Makokha, mmoja wa walionufaika, alipongeza mpango huo akisema utasaidia pakubwa katika kupunguza mateso ya watoto wa mitaani katika eneo hilo.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!