Raila Aitaka IEBC Kufungua Sava

Kiongozi wa Azimio la Umoja Raila Odinga ametoa changamoto kwa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC kufungua sava iwapo wanahisi matokeo yaliyotangazwa hadharani na mtoa taarifa si sahihi.
Raila anashikilia kuwa William Ruto hakushinda uchaguzi wa urais wa Agosti 9 2022 na kwamba muungano wa Azimio la Umoja One-Kenya haumtambui kama rais wa Kenya.
Anasema katika siku zijazo watachapisha matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9 kwa mujibu wa katiba ili Wakenya wajue ni nini hasa kilifanyika baada ya kupiga kura zao.
Akizungumza mjini Busia Jumapili, Odinga alisema kilichochapishwa ni matokeo ya kila kaunti ambayo hayajaainishwa kisheria.
Raila aliandamana kwenye mkutano wa Busia na miongoni mwa viongozi wengine, mgombea mwenza wake katika uchaguzi uliopita, Martha Karua, Kalonzo Musyoka, Wycliffe Oparanya, George Wajackoyah miongoni mwa wengine.
Kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua pia alilitaka shirika la uchaguzi-IEBC kufungua sava yake kwa uchunguzi huku kukiwa na ripoti ya mfilisi iliyowasilisha matokeo tofauti ya uchaguzi wa Agosti.
Karua pia aliukabili utawala wa Kenya Kwanza, akidai kuwa licha ya kukusanya takriban trilioni 1 za ushuru tangu waingie mamlakani, Wakenya bado wanateseka kutokana na njaa na gharama ya juu ya maisha.