‘Usaliti hautavumiliwa!’ Raila Awaonya Wabunge Wa Azimio
Kiongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja One-Kenya Raila Odinga amekariri kuwa muungano huo hautamtambua Rais William Ruto kama kiongozi aliyechaguliwa kihalali nchini.
Katika taarifa iliyotolewa baada ya mkutano wa siku mbili wa kundi la Azimio Bungeni mjini Machakos, Odinga ametuma ujumbe wa onyo kwa wanachama wa muungano huo, akisema kuwa aina yoyote ya usaliti haitavumiliwa.
Mkuu wa Azimio amekariri Ikulu kwamba ina fedha stahiki hivyo Wabunge wa Azimio hawapaswi kudai kuwa wanatafuta fedha za maendeleo katika ushirika wao na rais.
Badala yake amewatahadharisha wabunge dhidi ya kutumbukia katika siasa za ‘uhujumu’ ambao unaweza kudumaza utoaji wao wa huduma na uwakilishi wa wapiga kura wao.
Hisia za Odinga zimejiri baada ya baadhi ya wabunge wanaounga mkono muungano huo kufanya mkutano na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi.
Wabunge hao ni pamoja na; Seneta wa Kisumu Tom Ojienda, Wabunge Felix Odiwuor (Langata), Mark Nyamita (Uriri), Caroli Omondi (Suba Kusini), Gideon Ochanda (Bondo), Elisha Odhiambo (Gem), Paul Abuor (Rongo) na Walter Owino (Awendo).
Siku ya Alhamisi, Waziri Mkuu huyo wa zamani aliwataja viongozi hao kama wasaliti huku akitaka wajiuzulu akitaja hatua hiyo kama ‘ukahaba wa kisiasa’.