Home » Mzozo Wa Uteuzi Wa MCAs Murang’a Waendelea

Walalamishi ambao walikuwa wamewasilisha kesi ya kutaka kufutwa kwa uteuzi wa wawakilshi wadi 12 katika Bunge la Kaunti ya Murang’a wameelezea kutoridhishwa kwao na uamuzi wa mahakama uliobatilisha wawili pekee katika orodha hiyo, wakiapa kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

 

Walalamishi wamesema walitaka orodha nzima ya wawakilishi wadi waliopendekezwa katika orodha ya juu ya jinsia na makundi yaliyotengwa kutupiliwa mbali lakini ni wawili pekee waliotupwa nje na mahakama.

 

Mmoja wa walalamishi hao Rose Muthoni kutoka Gatanga alisema uamuzi huo haukuwa wa kuridhisha na wanataka kukata rufaa dhidi ya kesi hiyo.

 

Amedai kuwa yeye ni miongoni mwa watu walioteuliwa kupitia orodha hiyo ambayo ilitolewa na viongozi lakini majina yao yalibadilishwa na kuwekwa watu wengine.

 

Joseph Munyao kutoka Ithanga alisema ikiwa mahakama iliona wawakilishi wawili hawakufaa, ina maana hata wengine hawakushikilia nyadhifa hizo.

Alisema utaratibu huo huo ulitumika kuteua wawakilishi wadi wote na hivyo hakuna hata mmoja wao aliyepaswa kuachwa.

 

Kieru Ndichu, mwenyekiti wa UDA huko Gatanga alisema mchakato mpya wa uteuzi unapaswa kufanywa, na wale wanaostahili kuchukua nafasi hizo.

 

Alisema katika orodha hiyo, watu waliotengwa na wachache hawakuwakilishwa na kuongeza kuwa mchakato unaofuata unapaswa kuwa wa uwazi.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!