Azimio Kuongoza Mkutano Kesho Kibra
Muungano wa Azimio la umoja one-Kenya unaoongozwa na kiongozi wake Raila Odinga, unatarajiwa kufanya mkutano mkubwa wa kupinga baadhi ya hatua za serikali kesho Jumapili Kibra jijini Nairobi.
Odinga amekuwa akiwaongoza wafuasi wake kutaka Rais William Ruto ajiuzulu baada ya kudai kuwa kura zake ziliibwa wakati wa uchaguzi wa 2022 licha ya Mahakama ya Juu kutupilia mbali kesi yake.
Ikumbukwe kwamba awali, alifanya mikutano katika uwanja wa Kamukunji na Jacaranda mnamo Januari ambapo aliapa kutomtambua Rais Ruto kama rais, akisisitiza kuwa kura hiyo iliibwa.
Rais Ruto na washirika wake wamepuuzilia mbali msukumo wa hivi punde wa Odinga kuwa ni upotevu wa muda, wakisema madai yake kuhusu wizi wa kura yamechelewa kidogo kwa sababu alikuwa katika Mahakama ya Juu muda wote.
Kiongozi huyo wa upinzani amewaacha wengi wakikisia juu ya mpango wake halisi wa mchezo na kile anachofanya, baada ya kutangaza kuwa havutii kupeana mkono na Ruto.
Mnamo Alhamisi, Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) ilimtaka Odinga kusitisha mikutano ya kisiasa inayoendelea ikisema inachochea matamshi ya chuki na kuiweka nchi katika hali ya wasiwasi.