Maafisa Saba Kaunti ya Nakuru Wakamatwa

Maafisa saba wa sasa na wa zamani wa Kaunti ya Nakuru wametiwa mbaroni hiyo jana kwa kupeana zabuni ya shilingi milioni 7.9 ya ujenzi wa Soko la Karatina.
Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi EACC inasema washukiwa watatu zaidi wanafuatiliwa kuhusiana na madai hayo.
Saba hao ni pamoja na bintiye aliyekuwa Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri, Edith Wanjiru ambaye aliwahi kuwa Afisa Mkuu wa Biashara, Ustawishaji Viwanda, na Utalii chini ya utawala wa Aliyekuwa Gavana Lee Kinyanjui.
Wale ambao bado wameajiriwa na kaunti hiyo ni pamoja na maafisa wa ununuzi Jackson Maingi na Anne Njeri, mhasibu Nickson Kibet na afisa wa utalii Florence Karanja ambaye alifanya kazi chini ya idara ya biashara.
EACC pia iliwakamata Edith Wangari na Jane Njoki ambao ni wakurugenzi wa Levi Contractors, kampuni iliyotoa zabuni hiyo.
Mkurugenzi wa EACC wa bonde la ufa (Ignatius Wekesa) alisema kuwa mwanakandarasi huyo hakuwa amesajiliwa na Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi (N.C.A) na alikosa kuwasilisha Cheti halali cha Uzingatiaji Ushuru huku uchunguzi ukifichua kuwa cheti chake kilikuwa kimeisha muda wake kabla ya mchakato wa kutoa zabuni.