LSK Yakashifu Idadi Ndogo Ya Wanawake Uongozini
Chama cha Wanasheria nchini Kenya LSK kimekashifu idadi ndogo ya wanawake wanaopanda vyeo vya juu licha ya kufuzu kwa vyeti vyao.
Makamu mwenyekiti wa LSK Faith Odhiambo amesema kuwa idadi ya wanawake katika taaluma ya sheria inaongezeka, hata hivyo, kuna wanawake wachache wanaopanda katika nyadhifa za juu katika sekta ya sheria.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti kuhusu wanawake katika sheria na uongozi, Odhiambo amewataka wanawake zaidi kushika nyadhifa za kitaaluma, za juu na hata mahakamani.
Aidha alimtaja jaji mkuu Martha Karambu koome na naibu jaji mkuu kama mifano ya wanawake wenye nguvu nchini ambao mawakili wachanga na wanawake wasomi wanapaswa kutamani kuwa kama wao.
Alisema ingawa kuna wanawake wengi zaidi katika mahakama na bungeni, bado kuna wanawake wachache wanaotekeleza sheria.
Kulingana na Rose Wachuka wa Taasisi ya Wanawake wa Kiafrika (IAWL), ingawa kuna wanawake wengi zaidi wanaojiunga kitaaluma, bado kuna vikwazo vingi vinavyowazuia kupanda katika nyadhifa za juu.
Hata hivyo ameahidi kuwa taasisi hiyo itachunguza vikwazo hivyo ili kutoa mapendekezo ya kiprogramu ambayo yanaweza kuwasaidia wanawake kufikia nyadhifa za juu katika kila moja ya tasnia hizo.