Majambazi Wakamatwa Na Vifaa Vya Kielektroniki Githurai 44

Washukiwa watatu wa ujambazi walikamatwa usiku wa kuamkia leo jumanne baada ya maafisa wa polisi kuwapata wakiwa na vifaa vya kielektroniki vilivyoibiwa katika eneo la Githurai 44, Nairobi.
Francis Itaru, Joel Njoroge na John Warui walikamatwa kufuatia taarifa kwa maafisa kutoka kituo cha polisi cha Kasarani.
Taarifa kutoka kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) ilieleza zaidi kuwa polisi walikuwa wamejulishwa kuhusu magari mawili yaliyokuwa yakisafirisha vifaa vya kielektroniki vilivyoibwa na kisha kuuzwa kwa wafanyabiashara wa eneo hilo.
Watatu hao walikutwa wakiuza vitu hivyo kwa wachuuzi wa kielektroniki na upekuzi ulifanyika mara moja kwenye gari lao ambapo stika za kughushi namba, funguo kubwa, Laptop ya HP na zana mbalimbali za kuvunja nyumba zilipatikana.
Washukiwa hao wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kasarani wakisubiri kufikishwa mahakamani