Home » Rais Ruto Kuteua Jopo La IEBC

Miezi mitano baada ya Uchaguzi Mkuu, mchakato wa kuwaajiri Makamishna wapya wa tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC umeibua mzozo mpya wa kisiasa.

Huku nafasi sita zikiwa zimeachwa wazi katika IEBC, mwelekeo umeelekezwa kwa Rais William Ruto na watu atakaowateua kuunda Jopo la Uteuzi litakaloajiri makamishna wapya.

Mnamo Jumatatu, Rais Ruto, alianzisha mchakato wa kuwaajiri Makamishna wapya wa IEBC kujaza nafasi za kutoka kwa aliyekuwa Mwenyekiti Wafula Chebukati, na Kamishna Boya Molu na Yakub Guliye ambao muda wa miaka 6 umetamatika, pamoja na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Juliana Cherera, Francis Wanderi na Justus Nyang’aya waliojiuzulu ili kuepuka kukabili mahakama inayoongozwa na Jaji wa mahakama ya Rufaa Aggrey Muchelule.

Kamishna Irene Masit, kwa upande wake, amesimamishwa kazi akisubiri mahakama kuamua hatma yake.

Sheria ya Marekebisho ya IEBC 2022 iliyotiwa saini na Rais Ruto inaeleza jinsi nafasi 7 katika Jopo la Uteuzi zitakavyoshirikiwa.
Sheria hiyo mpya imetenga nafasi mbili kwa Tume ya Huduma za Bunge na Baraza la Kidini, huku Tume ya Utumishi wa Umma, Kamati ya Uhusiano ya Vyama vya Kisiasa na Chama cha Wanasheria wa Kenya (LSK) itateua mjumbe mmoja kila mmoja kwenye jopo hilo.

Aidha hatua hiyo imepingwa vikali na Kinara wa muungano wa Azimio la Umoja One-Kenya Raila Odinga akisema lina mwelekeo wa kumpendelea Rais.

Mwanachama wa JLAC na Mbunge wa Mugirango Magharibi Steve Mogaka anasema: “Mchezaji mmoja anapochagua waamuzi wengi, basi hakuna haja ya kushiriki katika mchezo huo kwa sababu ni sawa. Mchezo lazima usimamiwe na timu ya haki, iliyochaguliwa kwa haki na kuwaridhisha wachezaji wote.”

Mbunge wa Tharaka George Murugara, ambaye ni Mwenyekiti wa JLAC, kwa upande wake anasema: “Ukweli ni kwamba tuko na katiba na sheria…sheria ifuatiliwe. Kutofautiana ni kawaida kwa sababu ni siasa, tutakuwa na maoni tofauti lakini mwisho wa siku, sheria lazima ifuatwe.”

Macho yote sasa yanaelekezwa kwa Rais ruto kutaja Jopo la Uteuzi litakaloajiri Makamishna wapya wa IEBC ambao watateuliwa kutegemea idhini ya Bunge.

Kamati ya Haki na Masuala ya Kisheria (JLAC) itakuwa na jukumu la kuwachunguza makamishna waliopendekezwa na kuwasilisha ripoti kwa kikao cha Bunge ili kuidhinishwa, kukataliwa au kufanyiwa marekebisho.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!