Watu Watatu Wafariki Kutokana Na Kipindupindu Wajir

/photo courtesy/
Wimbi la pili la mkurupuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika Kaunti ya Wajir limekumba maeneo ya Siriba na Biyamadhow na kuua watu watatu zaidi na kufanya idadi ya waliofariki kufikia tisa katika muda wa wiki mbili.
Aidha Wagonjwa sita walifariki wiki moja iliyopita katika kaunti hiyo.
Kituo cha matibabu ya kipindupindu cha Siriba kimesajili idadi kubwa zaidi ya wagonjwa, 135, huku 213 wakipatikana na ugonjwa huo huko Biyamadhow.
Akizungumza na jarida moja humu nchini, Mkurugenzi Mtendaji wa Afya Kaunti ya Wajir Habiba Ali, amesema kati ya vifo tisa, viwili vilitokea katika vituo vya matibabu, na waathiriwa wengine wanne walifariki kabla ya kulazwa katika kituo hicho.
Naibu Gavana wa Wajir Ahmed Mohamed amewaonya wakazi dhidi ya mila chafu na kuwaonya wagonjwa dhidi ya kutoroka kutoka kwa vituo vya matibabu kabla ya kuruhusiwa.
Wakati huo huo, wazee kutoka Siriba wameitaka kaunti hiyo kutofunga kambi ya Biyamadhow licha ya idadi ya wagonjwa waliolazwa kupungua hadi 13 wakionya kuwa hatua hiyo inaweza kutatiza vita dhidi ya ugonjwa huo.
Kulingana na serikali ya kaunti, hakuna sababu ya kutisha kwani wametuma wafanyikazi wa kutosha ambao wanaungwa mkono na wafanyikazi 11 waliotumwa na kituo hicho na Shirika la Msalaba Mwekundu.
Kando na kipindupindu, kaunti ya Wajir kwa sasa inapambana na mkurupuko wa ugonjwa wa kimeta na ukame mkali ambao umesababisha vifo vya mifugo.
Naibu Gavana wa Wajir anasema kaunti imeingiza pesa katika chakula cha msaada, uhamishaji pesa, usafirishaji mkubwa wa maji, hazina ya mzunguko, na programu za lishe shuleni ili kupunguza shida zinazoongezeka.