Home » Mombasa Kupata Sehemu Ya Mapato Ya Bandari

Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen amesema jopo kazi litaundwa kujadili mbinu zitakazohakikisha kaunti ya Mombasa inapata sehemu ya mapato yanayopatikana katika bandari ya Mombasa.

Murkomen amesema jopo hilo litajadili jinsi kaunti itanufaika na bandari bila kuongeza gharama ya kutumia kituo hicho na kulemea waagizaji.

Akizungumza mjini Mombasa, Murkomen alisema Rais William Ruto aliagiza wachukue hatua kwa kasi kuhakikisha kwamba Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari ya Kenya (KPA) inatoa pesa zinazohitajika kwa kaunti.

Hii inaashiria kuondoka kwa sera za serikali zilizopita ambazo zilikataa jaribio lolote la kaunti kutoza huduma za bandari ikidai kuwa litafanya kituo hicho kuwa ghali kwa waagizaji bidhaa, na kutokuwa na ushindani.

Gavana wa sasa wa kaunti ya mombasa Abdulswamad Nassir kwa muda wa miaka 10 iliyopita amekuwa na msukosuko wa kuanzishwa kwa ushuru huo akisema bandari hiyo ndiyo rasilimali kuu ya kaunti.

Nassir amefanya mikutano na Rais Ruto na naibu wake, Rigathi Gachagua, kujadili maendeleo ya Mombasa na njia za kuibua sintofahamu katika ugavi wa mapato ya bandari.

Katika mahojiano, Nassir alisema ushuru wa bandari unasaidia bajeti ya kaunti, na utatumika tu kwa maendeleo ya sekta muhimu kama vile afya, elimu, miradi inayofadhiliwa na maji miongoni mwa mengine.

Kulingana na Mswada wa Fedha, kwa sasa, katika Bunge hilo, Mombasa inataka kukusanya ushuru kutoka kwa magari yaliyoagizwa kutoka nje, makontena, mizigo iliyolegea, na huduma za afya kutoka kwa meli za humu nchini na kimataifa.

Mamlaka ya kaunti inataka kutoza ushuru wa bandari kwa kontena kwa kiwango cha takriban Sh 1,210) kwa kila futi 20 sawa na utozaji wa bandari kwa shehena iliyolegea kwa Sh 60 kwa tani.

Iwapo ushuru huo utakubaliwa na jopokazi hilo, basi Mombasa itakusanya mapato ya ziada ya Sh milioni  7.3 kutoka kwa makontena yanayohudumiwa bandarini kila siku.

Kaunti hiyo inalenga kutoza meli za kimataifa Sh 121,000 kwa huduma za afya bandarini huku meli za humu nchini zikilipa Sh 2,420 iwapo ushuru unaopendekezwa utaidhinishwa.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!