Home » Mhalifu Wa Mauaji Akiri Vihiga

Mwanamume mmoja kutoka kaunti ya Vihiga amekiri kumdunga kisu na kumuua mwanamke mwenye umri wa miaka 43 baada ya mtu aliyedaiwa kumkodi kutekeleza uhalifu huo kukosa kumlipa Ksh.20,000.

Mshukiwa huyo alijisalimisha kwa maafisa wa Kituo cha Polisi cha Mbale na kukiri kuhusika na mauaji ya mwanamke huyo Jumapili ya wiki iliyopita, aliyetambuliwa na polisi kwa jina moja  kama Kahongeri.

 

Kisa hicho kilitokea katika kijiji cha Sahini eneo bunge la Sabatia.

 

Kulingana na Kamanda wa Kaunti ya Vihiga Benjamin Ong’ombe, mshukiwa aliambia polisi kuwa alimdunga mwanamke huyo kisu shingoni kabla ya kumuacha kwenye jumba lililotelekezwa.

 

Mshukiwa ambaye alikamatwa mara moja hakufichua sababu ya mauaji hayo ambayo anasema yaliidhinishwa na mwanamke mwingine.

 

Ingawa awali walikuwa na shaka kuhusu madai ya mwanamume huyo, polisi walitembelea eneo la tukio na kugundua mwili wa Kahongeri ukiwa na silaha ya mauaji bado imekwama shingoni mwake.

 

Mwili wa marehemu umehamishiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya rufaa ya kaunti ya Vihiga huku mwanamke anayedaiwa kuamuru kuuawa kwa Kahongeri kwa sasa yuko chini ya ulinzi wa polisi.

Uchunguzi unaendelea kwa sasa.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!