Home » Wafanyakazi Posta hawajalipwa miezi 4

Picha kwa hisani. Moja yapo ya majengo ya Posta Kenya tawi la Kitale.

Na Burare Kennedy.

ZAIDI ya wafanyakazi 2,500 wa shirika la Posta nchini (PCK) ambalo limekuwa likikumbwa na changamoto za kifedha wanajiandaa kwa hali ngumu huku wakikosa mishahara yao kwa mwezi wa nne mfululizo.

Wafanyakazi hao walipokea mishara yao ya mwisho mwezi Septemba 2022.

Aidha, shirika hili limeshindwa kutimiza majukumu yake ya kifedha ikiwa ni pamoja na kulipa ushuru kwa Halmashauri ya ukusanyaji ushuru nchini (KRA) na ada zingine wanazokata wafanyakazi wao kama vile malipo ya uzeeni na mikopo ya benki.

Ripoti ya hivi majuzi ya Mkaguzi mkuu wa mahesabu Bi Nancy Gathungu imefichua kwamba shirika la PCK limezama katika madeni ya zaidi ya Sh2 bilioni.

Kinaya ni kwamba haya yakijiri, shirika hili pia linadai mashirika mengi ya serikali mabilioni ya pesa.

Shirika la PCK lilisambaza zaidi ya masanduku 46,000 ya upigaji kura katika vituo vya upigaji kura kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9 lakini bado linasubiri malipo.

Sasa muungano wa wafanyakazi unaitaka serikali ya Rais William Ruto kuvunjilia mbali bodi ya wakurugenzi na kumteua Afisa Mkuuu Mtendaji mpya.

Shirika hili aidha, linakamilisha shughuli za uteuzi wa mkuu mpya wa posta huku kipindi cha kuhudumu cha afisa mkuu mtendaji wa sasa Dan Kagwe kikitarajiwa kufikia kikomo mwisho wa mwezi Machi, baada ya kuhudumu kwa miaka mitano.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!