Raila Atangaza Maandamano Ya Saba Saba Kote Nchini Ijumaa
Kiongozi wa Chama cha Muungano cha Azimio La Umoja One Kenya Raila Odinga anasema maandamano yaliyopangwa kufanyika katika uwanja wa Kamukunji jijini Nairobi mnamo Ijumaa, Julai 7, 2023, yatafanyika nchini kote.
Akihutubia wanahabari kiongozi huyo wa Upinzani amewataka wafuasi wake wote kote nchini kuandamana siku ya kihistoria ya Saba Saba, kwa kupinga serikali iliyopo madarakani juu ya gharama kubwa ya maisha.
Odinga, ambaye aliahidi kuongoza mkutano mkuu katika uwanja wa Kamukunji, alisema atarasimisha mahali ambapo mikutano ya hadhara itafanyika nchini kote.
Kiongozi huyo wa Azimio alitaja ongezeko la ushuru wa bidhaa za matumizi, mafuta na upandishaji wa nauli uliotangazwa hivi majuzi, akibainisha kuwa mikutano ya mashauriano italenga kuususia utawala wa Rais William Ruto, sera na ushuru wake.
Alisema muungano wa upinzani utaongoza Wakenya katika ukusanyaji wa sahihi kukataa utawala.
Kwa hivyo, Waziri Mkuu huyo wa zamani aliwataka wananchi kuunga mkono hatua yake ya kupinga kile alichokitaja kama ‘udikteta’ na kukataa ushuru mpya uliotozwa ambao alisema umefanya maisha ya Wakenya kushindwa kuvumilika.