Wakenya Wakodolea Macho Maisha Magumu
Wakenya wanakodolea macho hali ngumu ya kiuchumi baada ya Wabunge wengi kuidhinisha pendekezo tata katika Mswada wa Fedha wa 2023 la kutaka Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye mafuta iongezwe kutoka asilimia nane ya sasa hadi asilimia 16.
Baada ya mabishano makali yaliyoshuhudia wabunge wa Azimio na Kenya Kwanza wakifungana bungeni, wabunge 184 walipiga kura ya kuunga mkono ongezeko la VAT hadi asilimia 16 dhidi ya 84 waliopinga marekebisho hayo, na kuweka mazingira yatakayopelekea kuongezeka kwa gharama ya mafuta. kwa zaidi ya Ksh.10.
Wabunge wa muungano wa upinzani wa Azimio ambao walipinga pakubwa pendekezo la kuongeza VAT kwa mafuta hadi asilimia 16 waliteta kuwa hatua hiyo itaathiri vibaya gharama ya maisha.
Mbunge wa Kitui ya Kati Makali Mulu ambaye alikuwa amefanya marekebisho ya kutaka Kifungu cha kuongeza VAT kwenye mafuta kifutwe kwenye Mswada wa Fedha wa 2023, alisema kuwa wakati wowote VAT ya mafuta inapoongezwa, husababisha gharama za juu za usafirishaji, utengenezaji, uzalishaji pia kama umeme.
Kinara wa walio wachache Junet Mohamed alitaja Kifungu cha kuongeza VAT kuwa “kinachochukiza zaidi” kwa Wakenya, akionya kuwa kinaweza kuwa kitangulizi cha mapinduzi nchini.
Aliendelea kushutumu serikali ya Kenya Kwanza kwa kuwahadaa Wakenya kwa kuahidi kurekebisha gharama ya mafuta kwa kupunguza ushuru.
Kiongozi wa wachache Opiyo Wandayi pia alipinga vikali pendekezo hilo, akisema kwamba jaribio lolote la kuongeza gharama ya mafuta litakuwa siku ya huzuni zaidi katika historia ya Kenya.
Wandayi alipuuza hoja ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kitaifa ya Fedha na Mipango Kuria Kimani kwamba VAT kwenye mafuta inapaswa kuongezwa ili kufikia kiwango cha bidhaa na huduma zingine zinazoweza kuuzwa.
Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba kwa mara nyingine alisisitiza msimamo wake kwamba licha ya kuchaguliwa chini ya Chama tawala cha UDA, hataunga mkono sheria yoyote ambayo ingewaelemea Wakenya.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Matumizi Ndindi Nyoro alipuuzilia mbali majaribio ya upande wa wachache kupinga pendekezo la kuongeza VAT kwenye mafuta, badala yake akawapa changamoto kutoa njia nyingine mbadala za kuongeza mapato.
Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah alikiri kuwa bei ya mafuta nchini Kenya itaongezeka kutokana na kupanda kwa VAT lakini akadai VAT bado itakuwa chini ikilinganishwa na nchi jirani.
Bunge kwa sasa linazingatia mapendekezo kadhaa ya marekebisho ya Muswada wa Sheria ya Fedha wa 2023 ambao kwa sasa uko kwenye Kamati ya Bunge zima kabla ya kupitishwa kuwa sheria.