Maina Njenga Amtaka Gachagua Kufikishwa Mahakamani
Aliyekuwa kiongozi wa Mungiki Maina Njenga anataka Naibu Rais Rigathi Gachagua aitwe mahakamani kwa kudharau wito wa mahakama.
Kiongozi huyo wa zamani wa kundi lililoharamishwa la uhalifu alifikishwa mbele ya mahakama ya Nakuru, ambapo alimshtumu Gachagua kwa kutoa maoni yake hadharani kuhusu kesi ambapo anakabiliwa na mashtaka kadhaa miongoni mwao akiwa mwanachama wa kundi la uhalifu uliopangwa.
Katika maombi yake kwa mahakama, Njenga aliiomba mahakama kumwita Gachagua, akipinga maoni ambayo ametoa kumhusu ni dharau kwa sababu suala hilo bado liko chini ya mahakama.
Maombi ya Njenga hata hivyo yalikataliwa huku mahakama ikisema haikuridhika kuwa kweli kulikuwa na ukiukaji.
Awali Njenga amekashifiwa kwa tuhuma za kuhutubia mkutano katika eneo la Wanyororo katika Kaunti ya Nakuru mnamo Mei 11, 2023, “kuhimiza uungwaji mkono” kwa kundi lililoharamishwa la uhalifu, Mungiki.
Aidha anakabiliwa na mashtaka ya kujihusisha na uhalifu. Anadaiwa kuwaalika watu binafsi kwenye mkutano huo eneo la Wanyororo ambako anadaiwa kutoa maelekezo yanayohusiana na Mungiki.
Anashutumiwa pia kwa kumiliki “kamba ya mkoba wa kijeshi, mali ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) ambayo inashukiwa kuibiwa au kupatikana isivyo halali.”