Home » Kipindi Cha Dkt Patrick Njoroge Kama Gavana Wa CBK Chakamilika

Kipindi Cha Dkt Patrick Njoroge Kama Gavana Wa CBK Chakamilika

Muda wa miaka 8 wa Gavana wa Benki Kuu ya Kenya (CBK) Dkt. Patrick Njoroge ulikamilika hiyo jana Jumapili Juni 18, 2023.

 

Dkt. Njoroge aliteuliwa na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta mwezi Juni, 2015 kuhudumu kwa muda wa miaka minne huku muda wake katika usukani wa CBK ukiongezwa mara moja, Juni, 2020, kulingana na sheria iliyowekwa.

 

Nafasi yake itachukuliwa na Naibu Waziri wa zamani wa Hazina Dkt. Kamau Thugge ambaye ataanza kazi Jumatatu.

 

Dkt Thugge aliteuliwa Jumanne iliyopita na Rais William Ruto baada ya uteuzi wake kuangaziwa na bunge.

 

“Katika kutekeleza mamlaka yaliyotolewa na kifungu cha 13 (1) cha Sheria ya Benki Kuu ya Kenya, mimi, William Ruto, Rais wa Jamhuri ya Kenya na Kamanda Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi namteua Dkt. Kamau Thugge kuwa Benki Kuu ya Kenya, kwa muda wa miaka minne, kuanzia tarehe 19 Juni, 2023,” Rais Ruto alisema katika Notisi ya Gazeti la tarehe 13 Juni, 2023.

 

Na huku muhula wake ukikamilika, Dkt Njoroge anasema amefurahia kuwatumikia Wakenya katika wadhifa huo.

 

“Leo ni siku yangu ya mwisho kama Gavana wa Benki Kuu ya Kenya (CBK), nikifunga sura iliyoanza miaka minane iliyopita. Ukweli usemwe, imekuwa heshima kuu kuhudumu kama Gavana wa CBK,” Dkt. Njoroge anasema huku akikaribia kuondoka.

 

Anasema anajivunia utendakazi wake wa hali ya juu ambao unadhihirishwa na sekta ya benki ambayo imeimarika na kupanuka pakubwa, ikiwa na miundo bora ya biashara, umakini wa wateja, na benki zinazofanya kazi na Wakenya.

 

Hata hivyo, kwa Gavana anayekuja Dk. Thugge, anasema mengi zaidi bado yanafaa kufanywa akimuonya kwamba jukumu analokaribia kulichukua ni mbio za muda mrefu.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!