Sifuna: ODM Itawafukuza Wabunge Waliosusia Kupiga Kura Kwa Mswada Wa Fedha
Katibu Mkuu wa Orange Democratic Movement (ODM) Edwin Sifuna amesema kuwa chama hicho kitawafukuza wabunge waliopuuza kupigia kura mswada tata wa Fedha wa 2023.
Bunge la Kitaifa Jumatano lilipiga kura 176 kwa 81 kuunga mkono Mswada huo kusomwa Mara ya Pili.
Mswaada unakuja kwa hatua ya Tatu ya Kusoma Jumanne ijayo.
Wakati wa kikao hicho, angalau wabunge 92 kutoka katika nyanja zote za kisiasa hawakuwapo huku wengi wao wakiwa wa muungano wa upinzani wa Azimio.
Akizungumza mjini Bungoma, Sifuna alifichua kuwa chama hicho tayari kimewakabidhi barua za kuwatimua wabunge hao ambao hawakuonekana katika shughuli za upigaji kura.
“Hatutaki waoga na wale ambao wanaweza kuhujumiwa kirahisi kupigia kura mswada huo, tayari tumewakabidhi barua za kufukuzwa,” Sifuna alisema.
Seneta huyo wa Nairobi alisema ODM haitatoa visingizio vyovyote kutoka kwa wabunge wanaolengwa.
Alisema kuwa jukumu la msingi la wabunge waliochaguliwa ni kusimama kidete Bungeni na kuwatetea wananchi dhidi ya mzigo wowote wa utawala wa Kenya Kwanza.
Alisisitiza kuwa upinzani utaendelea kutoa usimamizi mkali kwa utawala wa Rais Ruto.
Sifuna alitaja kisa cha kampuni ya sukari ya Nzoia ambayo utawala wa Ruto unadaiwa kutaka kubinafsishwa.
“Sisi ndio tulipiga kelele kuzuia kampuni ya sukari ya Nzoia isiuzwe kwa wawekezaji wa kibinafsi kwa hivyo tuna jukumu muhimu katika kulinda rasilimali zetu,” Sifuna aliongeza.
Seneta huyo wa jiji aliwalaumu wabunge wa Kenya Kwanza kwa kupinga nyongeza ya fedha kwa kaunti mbalimbali akibainisha kuwa maseneta wa Ruto walikataa mgao wa Sh407 bilioni kwa kaunti.
“Wabunge wa Kenya Kwanza ndio ambao hawataki kaunti zetu zipate mgao wa simba kwa sababu walipiga kura ya Hapana ili kaunti zipate Sh407 bilioni kutoka kwa hazina ya kitaifa,” akasema.
Sifuna alisema katika mwaka wa kifedha wa 2023-24, kaunti zimetengewa chini ya shilingi bilioni 407 kinyume na pendekezo la awali.