Okang’o:Mradi Wa Nyumba Utauendelea Iwapo Kila Kitu Kitakuwa Wazi

Katibu wa maswala ya kisiasa wa chama cha KANU Fred Okang’o ametoa changamoto kwa serikali kufafanua mpango wa Makazi wa bei nafuu kwa uwazi zaidi la sivyo hautatekelezwa.
Kulingana na Okang’o, serikali imekuwa na hali ya kutojua wazi jinsi mpango huo utakavyoendeshwa na hivyo kuzua tashwishi miongoni mwa Wakenya na viongozi wanaoupinga.
Akizungumza kwenye runinga hii leo Jumatatu, Okang’o amesema kwamba ikiwa serikali ingependa kuwafanya Wakenya wengi waamini katika mpango huo, wanapaswa kuacha lolote na kueleza jinsi ushuru wa lazima wa asilimia 3 utafanya kazi na jinsi Wakenya watafaidika nayo.
Okang’o ameongeza kuwa serikali inahitaji kushirikiana na wataalam kutoka sekta tofauti ili kusaidia kutoa ripoti ya kina ambayo itamgusa kila Mkenya wa kawaida.
Mpango wa Makazi ya Affordable Housing umekabiliwa na mzozo mkali kati ya watu tofauti nchini kwani wengi wamedai kuwa mpango huo nnjia ya ufisadi.
Maswali yanayojitokeza kwenye pendekezo hilo ni ‘Nani atajenga nyumba hizo, Kwa nini nichangie ikiwa tayari nina nyumba, Je! nikichangia na bado sipati nyumba itakuwaje? na Nani anasimamia michango?’
Rais William Ruto ameeleza kuwa Wakenya wanafaa kuchangia kwa sababu kuna haja ya kuwainua Wakenya walio chini kabisa kiuchumi hivyo basi ni kwa nini kila mtu anapaswa kuchangia kusaidia wale wanaoishi katika hali mbaya.
Kinara wa Wengi katika Bunge la Kitaifa na Mbunge wa Mugirango Kusini Sylvanus Osoro ametoa maoni kwamba mchango huo hautawekwa katika akaunti ya pamoja ya serikali bali utahifadhiwa na benki ya kibiashara na kusambazwa na msimamizi husika.
Waziri wa Biashara Moses Kuria kwa upande wake amesema kuwa mradi huo utaongozwa na serikali za kaunti na sio lazima serikali ya kitaifa ambapo Magavana 47 wataongoza mradi huo.
Naibu Waziri wa Makazi Charles Hinga pia amesisitiza kuwa serikali itatoa nafasi ya kurekebisha pendekezo hilo na mchango uliopatikana kwa muda wa wiki mbili za ushiriki wa umma.
Ushuru wa Nyumba upo katika Muswada wa Sheria ya Fedha wa 2023 ambao umepangwa kuwasilishwa Bungeni kwa mjadala.