Raila Kuongoza Maandamano Iwapo Mswaada Wa Fedha 2023 Utapitishwa

Siku chache kabla ya kuwasilishwa kwa Mapendekezo ya Muswada wa Sheria ya Fedha wa 2023 kwa usomaji wa pili Bungeni jumanne hhii, tayari kuna mvutano kati ya wanaoupinga na wanaouunga mkono.
Viongozi wa upinzani kutoka muungano wa Azimio la Umoja One-Kenya wameonya kuhusu kurejeshwa kwa maandamano iwapo mapendekezo ya Mswada wa Fedha, 2023 utapitishwa.
Kiongozi wa Azimio Raila Odinga alikuwa katika Kaunti ya Bungoma Jumamosi, ambako aliendelea kupuuza mapendekezo yaliyomo kwenye Mswada huo ambayo anasema yatakuwa mzigo wa ziada kwa mlipa ushuru aliyeelemewa na mzigo.
Raila aliahidi kupigana ili kuhakikisha kuwa Mswada huo umemezwa na kimbunga cha upinzani mkali dhidi yake.
Kiongozi huyo wa upinzani, ambaye aliendeleza ukosoaji wake wa ushindi wa Rais William Ruto, alimshutumu Mkuu wa Nchi kwa kuendesha serikali inayoendeleza ukabila.
Maoni kama hayo yalitolewa na kiongozi wa chama cha Narc-Kenya Martha Karua ambaye alitaka kusimamishwa kwa Mswada huo, akiutaja kuwa kandamizi.
Katika Kaunti ya Makueni kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka alikuwa akisoma maandishi yayo hayo, akitishia kurejea kwa maandamano ya barabarani iwapo serikali itaendelea na mpango wake wa kupitisha Mswada huo.
Kalonzo alikuwa akizungumza wakati wa mazishi ya Monicah Kivatu, shangazi ya aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko, huku Kalonzo akitumia fursa hiyo kumwalika Sonko kwenye vuguvugu la upinzani.