Watu Wanne Wajeruhiwa Huku Mamia Ya Mifugo Wakiibwa Samburu
Watu wanne wamejeruhiwa na mamia ya wanyama kuibiwa huku majambazi wakivamia kijiji cha Lolmolog kaunti ya Samburu.
Majambazi walivamia kijiji hicho huku Waziri wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa Prof. Kithure Kindiki akizuru maeneo yanayokumbwa na majambazi katika kaunti za Baringo, Elgeyo-Marakwet na Pokot Magharibi.
Haya yamejiri wakati Kindiki alipotangaza kuanzishwa kwa shule tano za jumuiya katika eneo hili katika jaribio la kukabiliana na ukosefu wa usalama.
Viongozi kutoka jamii tatu zilizokuwa zikizozana hapo awali walikutana katika mkutano wa pamoja wa amani huko Chesegon katika makutano ya kaunti za Elgeyo Marakwet, Baringo na Pokot Magharibi.
Ulikuwa mkutano wa amani uliowaleta pamoja viongozi na wakazi kutoka jamii za Pokot na Marakwet.
Waziri huyo alitangaza kuwa serikali itaanzisha mara moja shule tano za jumuiya katika Mpango wa Elimu kwa Amani.
Shule hizo tano; Dira, Todo, Tuwit, Lomuke, na Chepchoren, zitatoa elimu ya lazima kwa wanafunzi kutoka kaunti za Elgeyo Marakwet, Baringo na Pokot Magharibi.
Huko Samburu, majambazi walivamia kijiji cha Lolmolog na kuwajeruhi wenyeji wanne, akiwemo afisa wa zamani wa kijeshi katika shambulio la Ijumaa asubuhi.
Wakaazi wa Lolmolog wamekashifu kile wanachodai kuzuka upya kwa ujambazi katika eneo hilo.
Waziri wa Mambo ya Ndani aliagiza kamati za usalama na kijasusi katika kaunti za Elgeyo Marakwet, Baringo na Pokot Magharibi kutambua, kufuatilia, kumkamata na kumfungulia mashtaka kiongozi yeyote anayechochea ghasia, chuki za kikabila au wizi wa mifugo, bila kujali itikadi zao za kisiasa.
Serikali kwa ushirikiano na washirika wa maendeleo itafufua mradi wa unyunyizaji maji mashambani kando ya Kerio Valley ili kuhimiza uvumilivu na utangamano baina ya jamii.