Mwalimu Afutwa Kwa Kula Ndizi, Kuku Ya Wageni

Mwalimu wa shule ya upili ya Nandi amezuiliwa na Tume ya Utumishi wa Walimu dhidi ya kuendelea na shughuli za kufunza kwa madai ya kula ndizi zote na kunywa maziwa katika ofisi ya Mkuu wa shule.
Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Lelmokwo anadaiwa kuvamia ofisi ya mkuu wa shule, akala ndizi na kuchukua maziwa yote.
Pia inadaiwa mwalimu alivamia jikoni na kulazimisha wapishi kumpa kuku aliyekusudiwa kuwa chakula cha wageni.
Katika barua iliyotumwa kwa mwalimu huyo na naibu mkurugenzi wa TSC kaunti ya Nandi W.O Mosigisi, alishtakiwa kwa kuvunja sheria.
“Nimeelekezwa na TSC kukuambia kuwa umekiuka Kifungu C (iii) na (iv) cha Jedwali la Tatu la Sheria.”
“Ulivamia ofisi ya mkuu wa shule mnamo Machi 15 mwendo wa saa 1.30 mchana bila ruhusa na ukala ndizi na maziwa yote kwenye friji,” Mosigisi alisema.
“Ulivamia jikoni la shule mnamo Machi 16 na kulazimisha wafanyikazi wa shule kukupakulia kuku ambao ulikusudiwa kwa wageni,” ilisema barua ya TSC.
Naibu mkurugenzi wa TSC, kwa hivyo, alimzuia mwalimu huyo kuanzia Mei 22.
“Kabla ya tume kutafakari na kuamua kesi yako, unaalikwa kutoa taarifa ya utetezi kwa tume kwa maandishi ndani ya siku 21,” naibu mkuu wa kaunti alisema.
Mwalimu pia alihakikishiwa kuwa ataruhusiwa kusikilizwa na tume.