Home » Nelson Koech Ashtumu Vyombo Vya Habari Kwa Kupotosha Umma

Nelson Koech Ashtumu Vyombo Vya Habari Kwa Kupotosha Umma

Mbunge wa Belgut Nelson Koech ameshutumu vyombo vya habari kwa kile anachodai kuwa kutoa taarifa potovu kwa umma’ kuhusu Mswada tata wa Fedha wa 2023.

 

Kwa maoni ya Koech, vyombo vya habari vimeibua mjadala kuhusu mswada huo, vikidai kuwa unawashawishi Wakenya wengi ambao hawajachukua muda wao binafsi kuupitia mswada huo.

 

Akiongea kwenye kipindi cha runinga moja hii leo Jumanne, Koech amedai kuwa vyombo vya habari vimewafumbia macho wale waliojitokeza kuunga mkono mswada huo na badala yake wamejikita katika kuwaripoti walioupinga.

 

Kulingana na Koech, mswada huo unajumuisha mapendekezo mengi mazuri ambayo yatawafaidi Wakenya, na vyombo vya habari vinafaa kujaza mianya inayosababisha pengo la habari.

 

Aidha amepongeza zoezi la ushirikishwaji wa wananchi ambalo anasema liliruhusu watu kutoa michango yao “pale wanapohisi kuwa jambo hili linakuja kuwaumiza wananchi.”

 

Mbunge huyo amekashifu upinzani ambao umejitolea kuhakikisha kuwa mswada huo unasambaratika bungeni, akiwataka wawape Wakenya nakala ya mswada huo.

 

Huku hayo yakijiri muungano wa Azimio la Umoja umeashiria kurejelewa kwa maandamano dhidi ya serikali iwapo mswada tata wa 2023 hautapitiwa upya, serikali inasalia na msimamo huku Naibu Rais Rigathi Gachagua akisisitiza kuwa mswada huo utapitishwa bungeni jinsi ulivyo.

 

Bajeti ya 2023/2024 imepangwa kuwasilishwa Bungeni Juni 15.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!