Home » Pokot Magharibi: Watoto Wawili Walazwa Hospitalini Baada Ya Kupigwa Risasi Na Majambazi

Pokot Magharibi: Watoto Wawili Walazwa Hospitalini Baada Ya Kupigwa Risasi Na Majambazi

Watoto wawili katika kaunti ya Pokot Magharibi wamelazwa hospitalini baada ya kupigwa risasi na watu wanaoshukiwa kuwa wavamizi kutoka kaunti ya Turkana.

 

Wavulana hao wenye umri wa miaka 11 na 10 walipigwa risasi baada ya kutekwa nyara na watu wanaoshukiwa kuwa wavamizi ambao waliwavizia walipokuwa wakichunga mifugo katika kijiji cha Kamurion kwenye mpaka wa Pokot Magharibi na Kaunti ya Turkana Jumamosi jioni.

 

Mashambulizi zaidi ya kulipiza kisasi yanaendelea kuripotiwa katika mpaka wa kaunti hizo mbili.

 

Haya yanajiri baada ya idadi isiyojulikana ya ng’ombe kuibwa kutoka kijiji cha Lochacha, eneo la Nasolot karibu na Sarmach Jumatano wiki jana.

 

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Chifu wa eneo la Kostei Afrikano Romano alisema watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi watano waliokuwa na bunduki walivamia kijiji cha Kamurio karibu na mbuga ya wanyama ya Nasolot na kuvamia kijiji hicho na kuwaondoa ng’ombe 100 waliokuwa wakichungwa na wavulana hao wawili.

 

Aliongeza kuwa wamiliki wa ng’ombe hao pamoja na wenyeji waliamua kufuatilia mifugo iliyoibiwa ndipo majambazi hao walipoamua kuwapiga risasi wavulana hao wawili.

 

Alisema kuna mvutano mkubwa katika eneo hilo na maafisa wa polisi wametumwa kudhibiti hali hiyo.

 

Kamishna wa kaunti ya Pokot Magharibi Apollo Okello alisema shambulio hilo lilifanyika Jumamosi alasiri na waliojeruhiwa wamelazwa hospitalini.

 

Alisema mmoja wa wavulana hao amelazwa katika hospitali ya rufaa ya Kaunti ya Kapenguria huku mwingine akipewa rufaa ya Moi Teaching na hospitali ya rufaa Eldoret kwa matibabu zaidi.

 

Kamanda wa polisi wa Kaunti Ndogo ya Pokot ya Kati Nelson Omwenga alisema wananchi walifanikiwa kupata mifugo iliyoibwa huku majambazi hao wakisambaratika kwenye eneo kubwa.

 

Alisema maafisa wa polisi wametumwa katika eneo hilo ili kupunguza hali ya wasiwasi.

Mabalozi wa amani katika eneo hilo wamekashifu visa hivyo wakitaka kuwepo kwa amani katika eneo hilo.

 

Rotich alitoa wito kwa Serikali kuharakisha kuweka kambi za kudumu za kijeshi katika eneo hilo ili kuleta suluhu la kudumu.
Alitoa wito kwa vijana kutoka jamii zinazozozana kukumbatia amani.

 

Mtaalamu Abel Lokwete alisema kuwa wanawake na watoto ndio wanaoathirika zaidi na ukosefu wa usalama.

 

Lokwete aliwataka wajumbe wa Kamati ya Amani ya Pokot na Turkana kuingilia kati suala hilo.

 

Zaidi ya watu 60 wameuawa na maelfu kuyahama makazi yao, mamia ya mifugo kuibiwa, na mali kuharibiwa katika eneo la Kerio Valley tangu mwaka huu uanze.

 

Uingiliaji kati wa kijeshi ili kukamilisha juhudi za polisi katika vita dhidi ya majambazi ambao wamesababisha ghasia na hasara ya mali katika eneo la North Rift haujazaa matunda kufikia sasa.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!