Wawakilishi Wadi Wa UDA Nakuru Wapuuza Agizo La Chama
Muungano wa Wanachama wa wawakilishi wadi Kaunti (AMCA) umepuuza agizo la uongozi wa Kenya Kwanza unaowaagiza kusitisha mpango wa kufungwa kwa mabunge ya kaunti.
Wawakilishi wadi wameapa kwamba wataendelea na mpango huo hadi madai yao ya hazina ya Wadi, usalama, pensheni na uhakiki wa mishahara yatakaposhughulikiwa kikamilifu.
Mapema wiki hii, Katibu Mkuu wa UDA Cleophas Malalah aliagiza Mabunge yote ya Kaunti iliyoshirikishwa na Kenya Kwanza kukoma kuwa sehemu za maamuzi ya wahusika wengine.
Malalah, katika barua aliwaagiza Viongozi wa Wengi katika mabunge kuhakikisha kwamba agizo hilo limefuatwa na kuripoti mwakilishi wadi yeyote aliyekiuka hili.
Lakini Katibu Mkuu wa AMCA Stanley Karanja amepuuzilia mbali vitisho hivyo akibainisha kuwa vita hivyo vilihusu ustawi wa wawakilishi na havina uhusiano wowote na vyama hivyo.
Mwakilishi wa UDA Wadi kutoka Naivasha Mashariki ameshutumu serikali kwa kuwapa mkataba akiongeza kuwa mabunge yote ya kaunti yatafungwa wiki ijayo.
Mwakilishi wadi huyo alisema kuwa wataendelea kusisitiza kuongezwa kwa mishahara yao kutoka KES86,000 hadi KES165,000 ya awali ambayo ilipunguzwa kutokana na maagizo kutoka kwa SRC.
Akizungumza mjini Naivasha baada ya mkutano wa mashauriano, Mmwakilishi wadi wa Viwandani Mwangi Muraya alimsuta Malalah na kuongeza kuwa wito wa malipo bora hauhusiani na chama.
Mwakilishi wadi wa UDA alibaini kuwa hakuna madai yao yoyote ambayo yameshughulikiwa na serikali na kusababisha mkwamo uliopo.
Haya yameungwa mkono na Mwakilishi wadi wa Eburru-Mbaruk Michael Gathanwa aliyesema kuwa hatua ya kupunguzwa mishahara yao ilinuiwa kuua ugatuzi.
Kwa upande wake, mwakilishi wadi wa Lakeview Alex Mbugua ameshangaa ni kwa nini serikali ilikataa kuwapa wawakilishi wadi pensheni ilhali viongozi wengine waliostaafu wananufaika.