Seth Panyako: Rais Ruto Alinifukuza Kutoka UDA

Makamu Mwenyekiti wa chama cha (UDA) Seth Panyako amedai kuwa Rais William Ruto alimwambia aondoke kwenye chama tawala.
Haya yanajiri baada ya Panyako kutangaza kujiuzulu kutoka kwa chama hicho siku ya Jumamosi, akitaja kile alichosema kuwa serikali ya Kenya Kwanza kugeuka ahadi ilizotoa kwa Wakenya wakati wa kampeni.
Panyako, akizungumza na waandishi wa habari, amedai kwamba kujiondoa kwake kutoka kwa chama kulilazimishwa na viongozi wa juu, akisisitiza kwamba jinsi ulivyoshughulikiwa ni kinyume na kanuni na sheria za chama.
Ameendelea kubainisha kwamba alipaswa kuitwa na kamati ya nidhamu ya chama, ambayo ilipaswa kumweleza makosa yake kabla ya kumruhusu kujitetea na uamuzi uliotolewa baadaye.
Kwa mujibu wa Panyako, yeye bado ni Makamu Mwenyekiti wa chama cha UDA kisheria licha ya kutangaza hadharani, hadi atakapowasilisha rasmi kujiuzulu kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa (ORPP) ambayo itazindua muundo mpya wa uongozi.
Amekashifu chapisho la mtandao wa kijamii la Katibu Mkuu wa UDA Cleophas Malala siku ya Jumamosi lililodai yeye hakuwa hata afisa wa chama kufuatia tangazo lake Jumamosi.
Panyako pia amepuuza ripoti kwamba alijiuzulu kutoka kwa chama kwa sababu alikosa uteuzi wa Baraza la Mawaziri.