Home » Raila Akosolewa Kwa Kutishia Ruto

Maoni ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga jana Ijumaa kugawa Kenya katika sehemu mbili yamezua hisia mseto miongoni mwa viongozi mbalimbali kote nchini huku wakosoaji wake wakimtaka kushinikiza umoja pekee.

 

Wakili maarufu, Profesa Patrick Loch Otieno (PLO) Lumumba, amemkashifu kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja, akidai kuwania mamlaka ndicho chanzo cha madai ya Odinga.

 

“Inasikitisha kwamba wakati raia wa nia njema wanafanya kazi kuelekea utangamano wa Afrika Mashariki (EA) na umoja wa Afrika, baadhi ya wanasiasa wa Kenya wanajadili kujitenga katika harakati zao za kupata nyadhifa za kisiasa.

 

Wakili wa katiba, Ahmednasir Abdullahi, pia amekubaliana na PLO Lumumba kwamba Raila alikuwa akitoa tishio hilo kwa madai ya kutaka mamlaka.

 

Itakumbukwa kwamba Saitabao Ole Kanchory, ajenti mkuu wa Raila wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2022, alitilia maanani suala hilo na kutupilia mbali kelele za kutaka kujitenga.

 

Raila na washirika wake kwa sasa wamempa Rais William Ruto wiki moja kukashifu madai ya naibu wake kuhusu Kenya kuwa kama kampuni hisa ambapo wanaofaidika ni wale waliowekeza pekee.

 

Raila alitoa kauli hiyo kwa Ruto alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa maombi ya kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka katika shamba la Yatta, Machakos jana Ijumaa.

 

Hata hivyo Rais William Ruto, alipokuwa akihutubia kikao cha pamoja cha wanahabari Jumapili, Mei 14, alikataa kukanusha matamshi ya naibu rais Rigathi Gachagua Mkuu huyo wa nchi, badala yake, aliwataka waandishi wa habari kumfikia Gachagua ili kupata ufafanuzi.

 

Gachagua, mnamo Februari 2023, alitangaza kuwa serikali itawapa kipaumbele wafuasi wake wakubwa wakati wa kufanya uteuzi na kutoa kandarasi, kauli ambayo ilizua taharuki na kuibua maswali kuhusu ukabila, upendeleo na ufisadi.

 

Wakati huo huo, hii si mara ya kwanza kwa Raila kutoa wito wa kujitenga katika msukumo wake wa kutaka serikali iwajibike ama kusalimisha matakwa yake.

 

Mnamo Oktoba 2017, Raila alitoa madai sawa na hayo ya kugawanya Kenya katika sehemu mbili, akitaja utawala mbaya wa Rais wa zamani Uhuru Kenyatta.

 

Raila alijiapisha kuwa rais wa wananchi Januari 30, 2018 huku Mnamo Machi 9, 2018, akifanya handisheki na Uhuru kwa kile kilichoitwa makubaliano ya kiungwana .

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!