Home » MCAs Waapa Kulemaza Shughuli Katika Mabunge Kote Nchini Kuanzia Jumatatu

MCAs Waapa Kulemaza Shughuli Katika Mabunge Kote Nchini Kuanzia Jumatatu

Muungano wa Wanachama wa Mabunge ya Kaunti (A.M.C.A) umeapa kulemaza shughuli katika mabunge yote 47 ya kaunti kuanzia Jumatatu wiki ijayo.

 

Hatua hii inajiri kufuatia kutokamilika kwa notisi ya siku 14 ambapo chama hicho kilikuwa kimeitaka serikali kushughulikia suala la mishahara yao, hazina ya wadi na usalama.

 

Notisi hiyo inajiri huku baadhi ya kaunti zikiwemo Garissa, Mombasa, Wajir na Mandera zikiwa tayari zimefunga mabunge yao kwa mijadala yoyote.

 

Kulingana na katibu mkuu wa chama hicho Stanley Karanja, wawakilishi wadi watahakikisha kuwa hakuna makadirio ya bajeti ambayo yatajadiliwa, hatua ambayo itaathiri utoaji wa huduma.

 

Aidha huyo mwakilishi wadi wa Naivasha Mashariki ameikashifu serikali ya kitaifa kwa kupuuza masaibu ya viongozi wa wadi na kuongeza kuwa hawatatishwa tena.

 

Akizungumza mjini Naivasha, Karanja amebainisha kuwa hakuna hata moja kati ya matakwa yao ambayo hadi sasa yameshughulikiwa na serikali na kusababisha mgogoro uliopo.

 

Kwenye hazina ya wadi, alisimulia mshangao wao wakati serikali iliposalimu amri na kukubaliana na hazina ya uangalizi ya Seneti na ongezeko la CDF kwa wabunge.

 

“Rais, Magavana, Maseneta, Wabunge na hata Wawakilishi wa Wanawake wana hazina iliyotengewa lakini kwa sababu zisizojulikana MCAs wamesahaulika,” alisema.

 

Mwakilishi wadi huyo amesema kuwa wataendelea kusisitiza kuongezwa kwa mishahara yao kutoka Ksh 86,000 hadi Ksh 165,000 za awali ambazo zilipunguzwa kutokana na maagizo kutoka kwa tume ya mishahara na marupurupu SRC.

 

Karanja ameongeza kuwa wawakilishi wadi wataendelea kutupilia mbali pendekezo lolote la bajeti linalolenga kuwagawia magavana pesa hadi matakwa yao yatimizwe.

 

Mwenyekiti wa hazina ya Bursary ya Naivasha Mashariki Phillip Waweru ameunga mkono wito wa kukagua nyongeza ya mishahara ya wawakilishi wadi kutokana na mahitaji mengi katika ngazi za mashinani.

 

Haya yameungwa mkono na kiongozi mwingine Mucoga Ng’ang’a ambaye alishangaa ni kwa nini MCAs, tofauti na viongozi wengine, wametelekezwa na kuongeza kuwa wanapaswa pia kupata pesa za wadi kama viongozi wengine.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!