‘Acheni Mchezo!’ Rais Ruto Awahutubia Wafanyikazi Wa KRA

Rais William Ruto amewaonya wafanyikazi wa almashauri ya Ukusanyaji Ushuru nchini KRA, dhidi ya kuendeleza ufisadi.
Kulingana na Rais Ruto kuna baadhi ya wafanyikazi wa KRA ambao wanashirikiana na watu wanaokwepa kulipa ushuru swala ambalo anasema limeathiri pakubwa pato la nchi.
Mkuu wa Nchi, ambaye alikuwa akizungumza hii leo Ijumaa katika eneo la Times Tower baada ya kuwasilisha ripoti zake za kodi, alibainisha kuwa ingawa mapato ya kodi yameongezeka kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni, msingi wa ushuru bado haujafikia uwezo wake kamili, akiilaumu KRA kwa matumizi yake akiitaja utumizi mbaya wa “teknolojia ambayo ni ya enzi ya zamani.”
Rais Ruto, ambaye alizungumza muda mfupi baada ya kuwasilisha rekodi yake ya ulipaji ushuru katika makao makuu ya KRA katika jumba la Times Tower jijini Nairobi, aliwahimiza wasimamizi wa KRA kuhakikisha kuwa halmashauri hiyo imepata sura mpya iwapo inapania kuafikia malengo yake katika ukusanyaji ushuru.
Ruto aidha aliahidi kuhakikisha uwajibikaji miongoni mwa wafanyikazi wa serikali wanapotumia fedha na mali ya umma.