Afisa Wa KDF Afariki Akisubiria Haki
Patrick Musyoka Ndana, afisa wa KDF na ambaye aligonga vichwa vya habari miezi mitatu iliyopita ambapo aliomba haki itendeke baada ya mkewe na mwanawe kuuawa kwa kukatwakatwa kinyama ameaga dunia.
Afisa huyo mwenye umri wa miaka 59 amezikwa karibu na kaburi la mkewe na mwanawe waliofariki baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana kwa tarehe tofauti nyumbani kwao.
Mkewe alivamiwa kwa panga nyumbani kwao Nguutani mnamo Oktoba 1, 2022.
Mwezi mmoja baadaye, mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 20 pia aliuawa baada ya kushambuliwa akiwa kwenye ardhi ya familia yao.
Marehemu alikuwa mgonjwa kwa miaka miwili na mauaji haya yote yalipotokea, alikuwa kwenye kitanda chake hospitalini.
Musyoka alikufa akiwa na hamu kwamba wauaji wa wapendwa wake watachukuliwa hatua.
Wenzake walimsifu Musyoka, ambaye alijiunga na vikosi vya Ulinzi mnamo 1986 kama afisa mchapakazi, mwaminifu na mzalendo aliyeshirikiana vyema na wazee na vijana wake.
Chifu msaidizi wa eneo hilo, Simeon Kavive alisema suala hilo linachunguzwa baada ya washukiwa kadhaa kukamatwa.
Kavive pia amewataka wenyeji kuacha kuishi kwa hofu kwani usalama umeimarishwa katika eneo hilo
“Tumeimarisha doria katika eneo hili kwa hivyo hakuna haja ya wenyeji kuishi kwa hofu,” Kavive alisema.
Msimamizi huyo aidha alikashifu vitendo hivyo vya kikatili akiwataka wenyeji kufanya kazi kwa karibu na uongozi ili kukabiliana kikamilifu na suala la ukosefu wa usalama.