Hofu Yatanda Katika Shule Ya Upili Ya Rapogi
Zaidi ya wanafunzi 100 kutoka shule ya Rapogi iliyoko Uriri huko Migori wamegundulika kuwa na dalili za mafua na hivyo kusababisha hofu katika taasisi hiyo.
Akithibitisha kisa hicho, Mwalimu mkuu wa shule hiyo Erastus Nyagwa amesema wanafunzi hao walioonyesha dalili za kikohozi kikavu na mafua walipelekwa katika hospitali mbalimbali za kaunti hiyo kwa uchunguzi na matibabu zaidi.
Nyagwa amesema kati ya vipimo Covid-19 imeondolewa kwa baadhi ya magonjwa yanayochunguzwa baada ya vipimo vilivyofanywa.
Hata hivyo, wanafunzi wawili ambao waligunduliwa na ugonjwa wa malaria walilazwa katika hospitali ya St Joseph Ombo huku wafanyikazi wote wa shule na wanafunzi wakiendelea kufanyiwa ukaguzi.
Nyagwa ametoa wito kwa shule mbalimbali kote nchini kuchukua tahadhari ili kuepekaha mkurupuko huo.
Huku msimu wa baridi ukiingia, Wakenya hivi majuzi wamekuwa wakilalamikia kukabiliwa na dalili mbaya za homa hiyo ikiwa ni pamoja na homa kali, kikohozi, , macho kutokwa na maji, kuumwa na kichwa na kuumwa mwili.
Homa ya mafua (mafua kamili) ni tofauti na homa na inaweza kusababisha ugonjwa mdogo au mbaya na kifo.
Watu wengi wanaopata homa hiyo hupona baada ya siku chache hadi chini ya wiki mbili, lakini baadhi ya watu hupata matatizo (kama vile nimonia), ambayo baadhi yake yanaweza kuhatarisha maisha.
Wakati uo huo, masomo katika Shule ya Sacred Heart Mukumu Girls katika Kaunti ya Kakamega yameanza tena huku zaidi ya wanafunzi 1800 kati ya 2028 wakiripotiwa kurejea kwa masomo.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Jane Mmbone aliiambia timu ya wakala mbalimbali ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Magharibi Samuel Irungu Macharia kuwa baadhi ya wanafunzi hao hasa wa kidato cha kwanza na cha pili wameomba uhamisho wa kwenda shule nyingine huku idadi ndogo ikitarajiwa kuripoti shuleni.
Timu ya wakala mbalimbali ilipewa jukumu la kutoa mapendekezo ya kuboresha usafi wa mazingira katika taasisi hiyo, hata hivyo imetangaza kuwa hakuna mlipuko mpya wa magonjwa katika taasisi hiyo, kinyume na taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Akizungumza na vyombo vya habari baada ya kufanya ziara ya kina shuleni hapo akiwa ameambatana na wajumbe wa timu ya mashirika mbalimbali miongoni mwao maafisa wa Wizara ya Maji, Afya ya Umma, wawakilishi wa wazazi na Mkuu wa shule, mkuu wa mkoa alizungumza juu ya madai potovu yanayohusu shule hiyo akiwataka kuwaruhusu wanafunzi kuzingatia masomo yao.
Hata hivyo mkuu huyo aliwaomba wazazi kuendelea kuwasiliana na wasimamizi wa shule kuhusu ustawi wa watoto wao na kuomba uungwaji mkono kutoka kwa washikadau wote ili kuhakikisha shughuli za masomo shuleni zinaendeshwa vizuri.
Shule hiyo ya Wasichana ya Sacred Heart Mukumu ilifungwa kwa takriban mwezi mmoja mwezi Aprili baada ya wanafunzi wanne na mwalimu kufariki kufuatia mkurupuko wa ugonjwa.
Maafisa wa afya ya umma waligundua salmonella typhii (bakteria inayosababisha typhoid) na amebiasis (maambukizi ya vimelea ya matumbo ambayo husababisha maumivu ya tumbo na kuhara).
Irungu alisema shule hiyo imeunganishiwa huduma mpya ya maji na Wakala wa Maendeleo ya Maji ya Ziwa Victoria Kaskazini ,mtambo mpya wa kusafisha maji na uwekaji wa klorini unaokaribia kukamilika na uanzishwaji wa vituo vya ziada vya kunawia mikono.
Akizungumzia mabadiliko ya asilimia 100 ya elimu ya sekondari, Mkuu wa Mkoa alibainisha kuwa yamekuja na changamoto miongoni mwao ni msongamano wa madarasa, mabweni na kuweka shinikizo kwenye mfumo wa maji taka shuleni.
Hata hivyo, alihakikisha kuwa Serikali imedhamiria kuboresha miundombinu shuleni kwa kushirikiana na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) na washirika wengine kuboresha miundombinu na usafi wa mazingira shuleni.