Home » Mahakama Yasusia Kufungua Akaunti Za Amadi

Mahakama Kuu imekataa kusitisha agizo la kufungia akaunti za benki za msajili mkuu wa Mahakama Anne Amadi na ile ya kampuni ya mawakili inayohusishwa naye ya kesi ya kashfa ya dhahabu ya Sh100 milioni.

 

Jaji David Majanja, ambaye alitoa agizo hilo wiki jana kufungiwa kwa akaunti za Bi Amadi na zile za Amadi & Associates, amekataa kuahirisha agizo hilo akisema haingefaa kuahirisha uamuzi huo, baada ya kujiondoa kwenye kesi hiyo.

 

Bi Amadi kupitia kwa wakili Ochieng Oduol ametaka agizo hilo lifutiliwe mbali akisema lilikuwa na chuki kwake kama msajili mkuu wa idara ya mahakama na hali hiyo ilimsababishia aibu ya kifedha kutokana na kushindwa kutimiza wajibu wake wa kifedha.

 

Jaji alisema alitoa maagizo hayo baada ya kushawishika kuwa Bi Amadi alisemekana kuwa wakili, lakini anafahamu kuwa hakuwa akitekeleza majukumu yake.

 

Alisema masuala hayo na mengine yatafikishwa mbele ya hakimu wa kitengo cha kibiashara (Jaji Alfred Mabeya) kwa maelekezo zaidi.

 

Raia wa Uingereza anayefanya biashara ya Bruton Gold Trading LLC alipata maagizo ya kufungia akaunti za benki za kampuni hiyo ya mawakili na za Bi Amadi, baada ya kudai kuwa aliibiwa zaidi ya Sh100 milioni za Marekani mwaka wa 2021.

 

Huku akitaka kusitisha agizo hilo, Oduol ameambia mahakama kuwa matukio yanayolalamikiwa yalianza mapema 2021 na “Tunaahidi kwamba akaunti hizo (za benki) hazitaingiliwa,”.

 

Lakini wakili Joseph Murage amepinga ombi hilo akisema kuwa kampuni ya mawakili ingali imesajiliwa kwa jina la Bi Amadi na maagizo yalitolewa ili kuhakikisha kesi hiyo ina msingi kwanza.

 

Bi Amadi, pamoja na mwanawe Brian Ochieng, Wakenya wengine wawili na raia wa Liberia wameshtakiwa na kampuni hiyo yenye makao yake makuu Dubai baada ya dhahabu iliyonunua kutofikishwa.

 

Demetrios Bradshaw alisema pesa hizo zilikusudiwa kwa ununuzi wa vyuma vya dhahabu, lakini madini hayo ya thamani hayakuwasilishwa kwa mnunuzi huko Dubai.

 

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Andrew Njenga Kiarie, Kikanae Topoti, Daniel Ndegwa Kangara almaarufu Daniel Muriithi na Edward Taylor almaarufu Mboronda Seyenkulo Sakor, mwenye hati ya kusafiria ya Liberia.

 

Ochieng (mtoto wa Amadi), Kiarie na Topoti ni mawakili katika kampuni ya mawakili, Amadi and Associates, huku Kangara akiwakilisha kampuni iitwayo Universal Gold Logistics Limited (UGL) na Sakor alisemekana kuwa mchuuzi wa dhahabu.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!