Mahakama Yasitisha Kamati Iliyobuniwa Kuchunguza Mauaji Ya Shakahola
Mahakama Kuu imesitisha shughuli za kamati iliyobuniwa na rais William ruto kutathmini hali ya mauji ya Shakahola katika kaunti ya Kilifi kwa siku saba kusubiri uamuzi wa kina utakaotolewa wiki ijayo.
Haya yanajiri baada ya muungano wa Azimio, unaoongozwa na kinara wa upinzani Raila Odinga, kushtaki kuuzuia kuanza vikao vyake kwa madai kwamba kamati haihusishi maoni ya umma na vile vile inatumia fedha kujinuisha wenyewe kwa kisingizio kwamba wanachunguza visa vya mauaji Shakahola.
Muungano huo uliwasilisha kesi hiyo wiki mbili zilizopita ukisema kuwa uteuzi wa Rais William Ruto wa timu hiyo ya wanachama wanane ni kinyume cha sheria na ni sawa na unyakuzi wa mamlaka yaliyopewa vyombo vingine vya serikali na Katiba.
Kulingana na Azimio, Rais Ruto alichukua mamlaka ya huduma ya polisi ya kitaifa NPS kufanya uchunguzi kwa kuteua kamati yake.
Zaidi ya hayo, muungano huo unadai kuwa hatua hiyo inadhoofisha amri ya Inspekta Jenerali wa polisi Japhet Koome, ambaye si tu kwamba anahitajika kufanya uchunguzi lakini pia haruhusiwi kuchukua maagizo kutoka kwa yeyote kuhusu nani wa kuchunguza.
Ombi hilo pia linamshutumu Rais Ruto kwa kuwapa uwezo wateule wake wa kibinafsi kuhujumu mamlaka ya kikatiba na mamlaka ya taasisi za kikatiba na vyombo vya serikali.
Rais Ruto aliteua kamati hiyo Mei 4 na kumteua jaji wa Mahakama ya Rufaa Jessie Lesiit kuwa mwenyekiti, kuchunguza vifo, mateso, unyama na udhalilishaji wa waathiriwa wanaohusishwa na Kanisa la Good News International huko Kilifi- wanaohusishwa na kasisi Paul Mackenzie.