Home » Mrembo Wa Benki Dubai Atembelea Kanisa La Ezekiel Kutafuta Mume

Mrembo Wa Benki Dubai Atembelea Kanisa La Ezekiel Kutafuta Mume

Mfanyakazi mmoja wa benki anayeishi Dubai ni miongoni mwa mamia waliomiminika katika Kanisa la Mchungaji Ezekiel Odero siku ya Jumamosi kutafuta upako wa kupata mchumba mwaume.

 

Josephine Mwatela ni mchanga, mwenye akili zaidi ya kibiashara na anatokea Taita Hills, lakini hajabahatika kupata mwanamume wa kumuoa.

 

Akiwa na umri wa miaka 33, Bi Mwatela alisema amezunguka ulimwengu na kuishi maisha ambayo wengi wanatamani ila bado hajapata tamanio la moyo wake.

 

Akiwa na kazi nzuri ya benki katika moja ya benki huko Dubai ambako anafanya kazi kama msimamizi mkuu, Mwatela anaonekana ameunda maisha yake vyema walakini, kama katika wimbo wa B2K ‘Girlfriend’, simulizi la Mwatela linafichua kuwa ana kila kitu isipokuwa mume.

 

Katika harakati zake za kutafuta nyota na mume wa kumuoa, alisafiri kutoka Dubai hadi Kituo cha Maombi cha Mchungaji Ezekiel kwa maombi huko Mavueni, Kaunti ya Kilifi.

 

Ni miongoni mwa wanawake waliofika kwa wingi wakitarajia kuombewa ili kupata wachumba.

 

Kulingana na simulizi yake mbele ya washarika mnamo Mei 13, alimwambia Mchungaji Ezekiel kwamba amechumbiana na wanaume kadhaa lakini kwa kawaida hukatisha uhusiano huo kila wachumba wanapopendekeza kumuoa rasmi dakika za mwisho.

 

“Naamini baada ya kuja hapa nitaweza kumpata mume wangu. Naamini Mungu anaweza yote. Nimekuwa nikichumbiana na wanaume tofauti lakini tatizo ni kwamba wanapopendekeza kunioa huwa nakatisha uhusiano huo. Hata hivyo, niligundua umri unanisonga na kuamua kuja kutafuta nyota yangu ili nipate mume,” alisema Mwatela.

Mwatela alisema aliokoka hivi majuzi na kuacha tabia yake ya kulewa pombe baada ya kukutana na kufanya ushirika katika kanisa la Ezekiel baada ya kumfuatilia kwa muda nje ya nchi.

 

“Nilikuwa nikinywa pombe na kutembea sana, lakini tangu nilipookoka na kuanza kufuata mahubiri ya Mchungaji Ezekiel, nimebadilika na ninaweza kwenda dukani na kunywa vinywaji vingine,” alisema Mwatela.

 

Huduma ya Mchungaji Ezekieli inaendelea kuvutia wanawake wengi, vijana na wazee ambao wanatafuta wenzi wa maisha.

 

Mmoja wa wanawake hao alikiri kuwa licha ya kuwa mrembo na mwenye tabia njema, ameendelea kuwavutia wanaume wanaomchezea tu hisia na kumtelekeza.

 

Katika mahubiri yake, Mchungaji Ezekieli alisema kufika madhabahu ya juu kutafuta mabadiliko ya maisha ili kufanikiwa kunakuja na jukumu kubwa linalohitaji uvumilivu.

 

“Mtumikieni Bwana kwanza na mengine yatafuata. Uvumilivu ni muhimu sana. Madhabahu ya juu ndipo tunapokuja kubadilisha maisha yetu na inakuja na uwajibikaji na changamoto kubwa,” alisema Ezekiel.

 

Licha ya utata unaotikisa huduma yake na kuchunguzwa, Mchungaji Ezekiel ameendelea kupokea wafuasi kutoka nchi za Uganda, Tanzania, Ghana, Dubai, na Australia.

 

Wengi huja kuombewa ili kuponywa magonjwa mbalimbali kama vile Ukimwi, kisukari, magonjwa ya akili, ulemavu wa mwili na kifafa.

 

Akina mama kwa usawa huja kusali na kutafuta nyota ya mafanikio kwa watoto wao; ili wafanye vyema shuleni na kuachana na dawa za kulevya.

 

Wengine hutafuta nyota ili kuwasaidia kufanikiwa katika biashara zao ambazo zimedorora na wengine kuomba kuacha uraibu wa pombe.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!