Home » Kioni Kwa Kega: Uhuru Alifadhili Kampeni Zako Leo Hii Una Madharau

Kioni Kwa Kega: Uhuru Alifadhili Kampeni Zako Leo Hii Una Madharau

Aliyekuwa Mbunge wa Ndaragwa Jeremiah Kioni amemkashifu mwenzake wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Kanini Kega kuhusu tamko la kumfukuza kutoka chama cha Jubilee.

 

Kioni na Kega kwa sasa wako kwenye vita vikali kuhusu uongozi wa chama cha Jubilee, huku kila mmoja akidai kuwa Katibu Mkuu halali wa chama hicho.

 

Akihutubia wanahabari jana Ijumaa muda mfupi baada ya ripoti za kutimuliwa kwake pamoja na Makamu Mwenyekiti David Murathe na Mweka Hazina wa Kitaifa wa chama hicho Kagwe Gichohi, Kioni amepuuzilia mbali hisia za Kega zinazomshutumu kwa kumsaliti kiongozi wa chama chake, aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta.

 

Kioni ameonekana kumzomea Kega akidai kuwa Uhuru alifadhili kampeni za (Kega) 2022 na kumteua kuwa mmoja wa wabunge wa EALA, lakini badala yake sasa amempa kisogo aliyekuwa Mkuu wa Nchi na anamkejeli bila shukrani kuhusu uongozi wa chama.

 

Mbunge huyo wa zamani wa Ndaragwa vile vile amekashifu mrengo wa Jubilee unaoongozwa na Kega dhidi ya kujitenga na chama hicho kinyume na katiba bila mashauriano ya umma.

 

Ametoa changamoto kwa wabunge wote waliochaguliwa wanaotaka kujiunga na Rais William Ruto anayeongoza Kenya Kwanza badala yake warudi kwa wananchi na kutafuta kuchaguliwa kwa tiketi ya vyama vingine.

 

Kega Ijumaa ametangaza kuwatimua Kioni na Murathe kwa kile alichokitaja kuwa utovu wa nidhamu, kushindwa kuheshimu chama na pia kukataa kutekeleza majukumu ya chama.

 

Kwa hivyo ametupilia mbali mkutano uliopangwa wa (NDC) kama ilivyotangazwa na Uhuru Jumatatu akisema maamuzi yoyote yatakayofikiwa hayatakuwa ya lazima kisheria.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!