Pendekezo La KENHA Lapata Pingamizi

Azma ya Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu Nchini (KENHA) ya kujenga makao yake makuu mjini Nakuru imetatizwa na mzozo kuhusu umiliki wa kipande cha ardhi cha KSh 100M tume ya kupambana na ufisadi EACC imedai mahakamani.
Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imekuwa katika mzozo wa muda mrefu wa kisheria na Hillary Kipkorir kuhusu umiliki wa kipande cha ardhi kilicho katika eneo la London huko Kiamunyi.
Tume hiyo iliyowasilisha kesi mbele ya Mahakama ya Mazingira na Ardhi ya Nakuru, imemshtumu Kipkorir ambaye ni nduguye aliyekuwa Kamishna wa Ardhi Sammy Mwaita kwa kujinyakulia hatimiliki ya ardhi hiyo kinyume cha sheria.
EACC ilielekea mahakamani Aprili 2015 ikitaka kurejesha ardhi hiyo kwa niaba ya KENHA.
KENHA, katika maombi yake ya kuamuru kesi hiyo, imedai ardhi hiyo, ambayo awali ilikuwa chini ya Wizara ya Ujenzi, ilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa makao yake makuu.
Mahakama imesikia kwamba eneo hilo pia lilipaswa kuwa na majengo ya kudumu, ikiongeza kuwa serikali ya Kenya imekuwa ikitumia na kumiliki ardhi hiyo ambayo sehemu yake imeendelea tangu katikati ya miaka ya 1980 hadi sasa.