Azimio, Kenya Kwanza Yarejelea Mazungumzo

Kamati ya watu kumi na wanne inayojumuisha wawakilishi wa Kenya Kwanza na wale wa Azimio kujadili masuala tata yaliyoibuka na haswa kupanda kwa gharama ya maisha na marekebisho kwenye tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC imerejelea vikao vyake.
George Murugara wa Kenya Kwanza amesema wamekubaliana kufanya kazi kwa kutumia mfumo mseto ambao utatambua mchakato wa bunge na pia mazungumzo nje ya bunge ambayo yataruhusu watu nje ya bunge kutoa maoni yao na pia kama waandishi wa habari.
Kwa upande wake, kiongozi wa Azimio Otiende Amollo ambaye pia ni mbunge wa Rarieda, ameunga mkono maoni ya Murugara akisema wamthibitisha kuwa kama timu moja na wanafurahishwa na maendeleo ya mazungumzo.
Wakati uo huo, ameongeza kuwa wameunda timu ya wanachama 6, 3 kutoka kila upande, ambao wataanza kupigia debe suala tata kuhusu uundwaji upya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Azimio itawakilishwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, Seneta wa Kitui Enoch Wambua na Mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo.
Kenya Kwanza itawakilishwa na Seneta wa Bomet Hillary Sigei, Seneta wa Kakamega Boni Khalwale na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.