Gachagua Aahidi Msaada Kwa Miradi Ya Blue-economy
Naibu wa rais Rigathi Gachagua ameahidi uungwaji mkono wa serikali kwa miradi muhimu ya kukuza uchumi wa blue-economy nchini.
Gachagua amesema utawala wa Kenya Kwanza utashirikiana na Umoja wa Ulaya na kaunti za pwani ili kufungua uwezo wa sekta hiyo.
Akizungumza leo hii Jumatano katika hoteli ya Muthu Nyali Beach mjini Mombasa alipoongoza uzinduzi wa boti za uvuvi zilizonunuliwa kwa ushirikiano na Umoja wa Ulaya chini ya Mradi wa Go-Blue, Gachagua amesema wako tayari kutoa rasilimali na usaidizi unaohitajika ili kuhakikisha mafanikio ya uchumi yanaafikiwa.
Mradi wa Go-Blue ni ushirikiano kati ya serikali na Umoja wa Ulaya na unalenga kuimarisha uchumi huo wa nchi kupitia kuwawezesha wavuvi wa ndani.
Mwezi uliopita, naibu rais alizindua miradi kama hiyo huko Mvita kaunti ya Mombasa na Shimoni huko Kwale, yote yenye lengo la kufufua sekta hiyo ambayo ni eneo kuu la utawala wa Kenya Kwanza.
Hata hivyo alisifu mazungumzo ya mashauriano na magavana watano chini ya Jumuiya ya Kaunti Za Pwani, kwa kueleza utayarifu wa kufanya kazi na serikali.
Waziri waMasuala ya Bahari na uchimbaji wa Madini Salim Mvurya alisema Wizara inaweka mazingira mazuri kwa ukuaji wa sekta ya uchumi .