Home » Seneta Maina:Natarajia Upinzani Wampongeze Rais Ruto

Seneta mteule Veronica Maina anasema upinzani unapaswa kumpongeza Rais William Ruto kwa kile anachokiona kama kuchukua hatua za haraka kukabiliana na kashfa ya mabilioni ya ununuzi katika Shirika la Usambazaji wa Dawa nchini (KEMSA).

 

Jana jumatatu rais Ruto alibatilisha uteuzi wa bodi ya KEMSA huku kukiwa na uchunguzi wa madai ya ufisadi na usimamizi mbovu wa vifaa vya matibabu katika shirika hilo, ambao pia ulisababisha Mkurugenzi Mtendaji kusimamishwa kazi pamoja na wafanyikazi watatu.

 

Aidha baadhi ya viongozi wa upinzani wamepuuzilia mbali hatua hiyo, huku Naibu Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Robert Mbui akisema anafurahia sakata hiyo ilizuka wakati wa utawala wa Rais Ruto kwa sababu utawala wa Kenya Kwanza ulikuwa unadaiwa kunyooshea vidole utawala wa zamani wa Jubilee kutokana na kashfa sawia ya ununuzi wakati wa janga la korona.

 

Mbui, ambaye amekuwa na Maina kwenye kipindi kimoja cha runinga humu nchini, amesema ingawa hafurahii ufisadi katika mashirika ya serikali, anafurahi kwa sababu anatarajia kesi ya KEMSA kuwafanya wanasiasa wa Kenya Kwanza kuacha kile alichokiita michezo ya lawama.

 

Akijibu, Seneta Maina hata hivyo amepuuzilia mbali maoni ya Mbui akisema kuwa utawala wa Rais Ruto unahitaji kupongezwa kwa kujibu haraka kukabiliana na kashfa hiyo.

 

Maina amedai kuwa Kenya Kwanza ilishughulikia hali hiyo vyema zaidi kuliko utawala wa Rais Uhuru Kenyatta, ambapo Kenya ilipoteza Ksh B.2.3 katika kashfa ya ununuzi wa vifaa vya korona.

 

Kulingana naye, hatua ya rais Ruto ingefaa kuibua maafikiano katika mgawanyiko wa kisiasa.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!