Ruto Amteua Kamau Thugge Kuwa Gavana Wa Benki Kuu
Rais William Ruto amemteua aliyekuwa Katibu Mkuu wa Hazina Kamau Thugge kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Kenya (CBK).
Hii ni kabla ya kustaafu kwa Dkt Patrick Njoroge ambaye amekuwa gavana wa CBK tangu Juni 2015.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei, uteuzi wa Dkt Thugge umefuata mchakato wa kuajiri wenye ushindani mkali uliotekelezwa na Tume ya Utumishi wa Umma.
Katibu huyo huyo wa zamani kwa sasa ni mshauri mkuu na Mkuu wa Sera ya Fedha na Bajeti katika ofisi ya rais Yeye pia ni mjumbe wa Baraza la Kiuchumi la Ruto.
Thugge alikuwa akikabiliwa na mashtaka ya ufisadi pamoja na aliyekuwa Waziri wa Hazina Henry Rotich.
Aidha Alishtakiwa kwa kula njama za uhalifu wa kiuchumi, , matumizi mabaya ya ofisi, kutenda kosa la utovu wa nidhamu, kujihusisha na mradi bila mipango ya awali na kushindwa kuzingatia sheria na kanuni zinazohusiana na usimamizi wa fedha za umma.
Hata hivyo alishtakiwa pamoja na Rotich kwa kuongeza mkopo wa kibiashara wa ujenzi wa mabwawa ya Kimwarer na Arror huko Kerio Valley wa Ksh B .17.
Mashtaka ya Thugge, hata hivyo, yalitupiliwa mbali na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji mnamo 2021, na akafanywa shahidi wa Serikali dhidi ya Rotich kuhusu kashfa hizo.
Kabla ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu mnamo 2013, alifanya kazi kama mshauri mkuu wa uchumi katika Wizara ya Fedha kutoka 2010.
Pia alifanya kazi katika Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuanzia 1985 hadi 2010 ambapo alihudumu katika nyadhifa za Mchumi Mwandamizi, na Naibu Mkuu wa Idara.
Thugge ana shahada ya uzamifu ya Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha John Hopkins nchini Marekani.
Saa chache tuu…. Rais William Ruto amemfuta kazi Dkt Josephine Mburu kama Katibu Mkuu katika Wizara ya Afya na Viwango vya Kitaalamu.
Dkt. Mburu amerejeshwa nyumbani kutokana na mchakato mbovu wa ununuzi unaosimamiwa na Wizara ya Afya ambao uliiacha nchi ikikaribia kupoteza thamani ya Ksh. B 3.7 za vyandarua vya kupambana na Malaria kutoka kwa Global Fund.
Katika taarifa iliyotolewa leo hii Jumatatu, Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei pia ametangaza kuwa Rais Ruto pia amebatilisha uteuzi wa Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya usambazaji wa Dawa nchini (KEMSA) ambayo ilihusika na mchakato wa ununuzi mbovu. .