Home » Rais Ruto Avunja Bodi Ya KEMSA

Rais William Ruto amefuta uteuzi wa Josephine Mburu kama Katibu Mkuu wa Idara ya Afya ya Umma na Viwango vya Kitaalamu kutokana na madai ya ubadhilifu ndani ya Mamlaka ya Usambazaji wa Dawa nchini (KEMSA).

 

Katika taarifa iliyotiwa saini na Felix Koskei, Mkuu wa Wafanyakazi na Mkuu wa Utumishi wa Umma, rais pia amebatilisha uteuzi wa mwenyekiti na kuvunja bodi nzima.

 

Kwa hivyo, mkuu wa nchi amemteua Irungu Nyakera kuwa mwenyekiti wa bodi na kuunda upya bodi nzima na wateule wapya wanne ambao ni Hezbon Oyieko Omollo, Bernard Kipkirui Bett, Dkt Jane Masiga na Jane Nyagaturi Mbatia.

 

Rais pia amemsimamisha kazi Terry Ramadhani kama Afisa Mkuu Mtendaji wa KEMSA pamoja na wafanyikazi wengine wanane ambao ni Martin Wamwea na Lenson Kariuki.

 

Wengine ni pamoja na Pauline Duya ,Livingstone Njuguna Dkt. Charles Kariuki Chege Justus Kinoti ,Cosmas Rotich na Anthony Chege.
Kwa upande wake, amemteua Dkt. Andrew Mutava Mulwa kama Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa KEMSA.

 

Rais Ruto amewahakikishia Wakenya kuwa serikali yake imejitolea kujenga upya mfumo wa usimamizi wa ugavi wa KEMSA ili kuhakikisha ufanisi na uwajibikaji.

 

Habari hizi zinajiri huku Mfuko wa Kimataifa ukilazimika kughairi zabuni ya vyandarua ya Ksh B 3.7 kutokana na mchakato wa ununuzi usio wa kawaida wa KEMSA.

 

Hii ni baada ya shirika hilo la kigeni kugundua kuwa kampuni hizo tatu ambazo zilikuwa zimefuzu na KEMSA zilikuwa na zabuni zisizofaa…….. Zaidi ya hayo, makampuni ambayo yalikataliwa na KEMSA yalikuwa yamekidhi viwango vilivyohitajika.

About The Author

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!