Rais Ruto Awaomba Wakenya Msamaha
Rais William Ruto ameomba msamaha kwa uzembe uliosababishwa na maafisa wa polisi ambapo umechangia vifo vya zaidi ya watu 200 katika eneo la Shakahola kaunti ya Kilifi.
Katika mahojiano ya pamoja na vyombo vya habari na mashirika sita ya habari Rais William Ruto aliwaomba Wakenya msamaha kwa kile alichokitaja kuwa uzembe wa mamlaka husika katika eneo la Shakahola Kaunti ya Kilifi katika vifo visivyojulikana kwa zaidi ya watu 200.
Rais alisema baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa tume ya uchunguzi DCI na kikosi kazi kilichoteuliwa, watakaobainika kuhusika watawajibishwa kisheria.
Wakati huo huo, Mawakili wanaomwakilisha Mchungaji Ezekiel Odero sasa wanadai kuwa kuna jaribio la kutaka ahukumiwe katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC kule Hague.
Mawakili hao wanadai kuwa serikali imeenda mbali zaidi kumhusisha Ezekiel na mhubiri mwenye utata kutoka Malindi Paul Mackenzie ambaye kwa sasa shamba lake la ekari 800 ndio kiini cha uchunguzi wa uhalifu unaoendelea.
Mawakili hao wanadai kuwa Ezekiel analengwa na viongozi wa kidini.